2015-06-12 17:47:00

Waziri mkuu wa Poland akutana na kuzungumza na Papa Francisko mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 12 Juni 2015 amekutana na kuzungumza na Bibi Ewa Kopacz, Waziri mkuu wa Poland ambaye baadaye amekutana pia na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa. Katika mazungumzo yao, Baba Mtakatifu Francisko na mgeni wake wamejadili kwa kina na mapana kuhusu hija ya kitume inayotarajiwa kufanywa na Baba Mtakatifu nchini Poland, hapo mwakani kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani.

Wamebainisha mchango mkubwa unaoendelea kutolewa na Kanisa Katoliki kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Poland katika ujumla wao. Wamegusia masuala ya kimaadili, kiuchumi na kijamii katika ulimwengu mamboleo. Baadaye, viongozi hawa wawili wamegusia pia masuala ya kimataifa, lakini kwa namna ya pekee hali ya usalama nchini Ukraine.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.