2015-06-12 17:29:00

Uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Hungaria na Vatican unaendelea kuboreka zaidi


Imekwishagota miaka 90 tangu Hungaria na Vatican walipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia na baadaye uhusiano huu ukavunjika na kudumaa kwa takribani miaka 45, leo hii ni miaka 25 tangu mahusiano haya yaliporejeshwa tena hapo tarehe 7 Februari 1990 kutokana na juhudi zilizofanywa na Kardinali Agostino Casaroli, aliyekuwa Katibu mkuu wa Vatican kwa wakati ule. Tangu wakati huo, kumekuwepo na maendeleo makubwa hasa katika uhuru wa kuabudu na urafiki kati ya nchi hizi mbili kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu nchini Hungaria.

Madhulumu ya Kanisa yalianza kunako mwaka 1945 kwa Serikali ya Hungaria kuanzisha mapinduzi ya kilimo yaliyosababisha Kanisa kunyang’anywa ardhi yake; shule zitakataifishwa na vyombo vya mawasiliano vilivyokuwa vinamilikiwa na kuendeshwa na Kanisa vikazuiwa kutekeleza wajibu wake kwa umma. Kunako mwaka 1950, Mashirika ya kitawa na kazi za kitume, yakapigwa marufuku kutekeleza utume wao nchini Hungaria na Vatican ikanyimwa haki ya kutekeleza utume wake katika maisha na ustawi wa Kanisa nchini Hungaria hususan katika uteuzi wa Maaskofu wa Makanisa mahalia.

Hii ni sehemu ya historia fupi iliyotolewa na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher wakati huu Hungaria na Vatican wanapoadhimisha kumbu kumbu ya miaka 90 ya uhusiano wa Kidiplomasia na Miaka 25 tangu uhusiano huu uliporejeshwa tena. Anasema, kunako mwaka 1964, Hungaria na Vatican wakatiliana sahihi Protokali iliyotambua dhamana na nafasi ya Vatican kwa Makanisa mahalia, hatua iliyopelekea kuteuliwa kwa Maaskofu kadhaa kwa ajili ya Majimbo Katoliki nchini Hungaria.

Kunako mwaka 1990, Hungaria na Vatican wakafungua ukurasa mpya kwa Vatican kuanzisha Ubalozi wake nchini Hungaria, maisha na utume wa Kanisa yakaendelea barabara kadiri ya Sheria za Kanisa kwa kuzingatia uhuru wa dhamiri pamoja na uhuru wa kuabudu; mambo ambayo yalikuwa yamezuliwa kabisa wakati wa utawala wa Kikomunisti.

Kunako mwaka 1994 anasema Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Hungaria na Vatican zikatiliana sahihi mkataba wa ushirikiano katika masuala kadhaa yaliyopania kukuza mafao ya pande hizi mbili. Kanisa likapewa uhuru wa kutekeleza dhamana yake katika huduma za kijamii hususan katika sekta ya elimu kwa kukazia tunu msingi za maisha ya kimaadili na utu wema; haki na amani pamoja na uzalendo, mambo ambayo hadi sasa ni sehemu ya mapokeo ya wananchi wa Hungaria. Mwaka 1997, taasisi za elimu zilizokuwa zinamilikiwa na kuendeshwa na Kanisa zikapewa hadhi sawa na taasisi za elimu zilizokuwa zinamilikiwa na Serikali, kwa kutoa ruzuku kwa Kanisa ili kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara. Mkataba wa mwaka 2013 ukafanyiwa marekebisho na kuridhiwa tena kunako mwaka 2014.

Tangu wakati huo, kumekuwepo na mahusiano mema kati ya Vatican na Hungaria kwa kujikita katika urafiki unaoambata majadiliano katika ukweli na uwazi, daima kwa ajili ya mafao ya wengi. Kanisa linapenda kuwakirimia watu matumaini na maisha ya uzima wa milele kwa njia ya huduma makini zinazogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Lengo ni kuendeleza ushirikiano kati ya watu wa Mataifa kwa ajili ya mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.