2015-06-12 16:58:00

Mateso na mahangaiko ya Wakristo huko Mashariki ya Kati kujadiliwa kwa kina


Mkutano mkuu wa themanini na nane wa Mashirika ya Misaada kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, ROACO itakuwa ni fursa makini kwa ajili ya kufanya upembuzi wa kina kuhusu mahangaiko na mateso ya Wakristo huko Syria na Iraq na jinsi ambavyo Kanisa linaweza kusaidia kuwahudumia watu wanaoteseka na kuhangaika kutokana na nyanyaso, dhuluma na mauaji yanayoendelea huko Mashariki ya Kati.

Katika mkutano huu, viongozi wakuu kutoka Vatican wanatarajiwa kushiriki na kutoa mada na kwa namna ya pekee, mada itakayowasilishwa na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican; Askofu mkuu Mario Zenari, Balozi wa Vatican nchini Syria pamoja na Askofu mkuu Giovanni Pietro dal Toso, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa linaloratibu na kusimamia misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum. Wajumbe watasikiliza taarifa ya hija ya kichungaji iliyofanywa hivi katibuni huko Mashariki ya Kati na Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki.

Awamu ya pili ya mkutano huu itajadili pamoja na mambo mengine hali ya Wakristo nchini Ethiopia, mada itakayopembuliwa na Kardinali Berhaneyesus Demetrew Souraphiel, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Addis Ababa ambaye pia ni Mwenyekiti wa AMECEA. Kutakuwepo pia na maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu, hapo tarehe 16 Juni 2015 kwenye Kanisa la Mtakatifu Stefano mjini Vatican kwa ajili ya kuombea amani huko Mashariki ya Kati na Ukraine. Ibada hii itaongozwa na Kardinali Leonardo Sandri.

Awamu ya tatu ya maadhimisho ya mkutano huu itajadili kwa kina na mapana hali ya Kanisa la Warmeni Wakatoliki Ulaya ya Mashariki, Georgia na Russia. Hapa wajumbe watapembua kwa kina na mapana hali ya maisha na utume wa Kanisa katika nchi hizi, utekelezaji wa miradi mbali mbali inayogharimiwa na Kanisa kutokana na mchango ya waamini Siku ya Ijumaa kuu. Viongozi kadhaa kutoka kwenye Makanisa ya Mashariki wanatarajiwa kuhudhuria na kwamba, mkutano huu unatarajiwa kufunguliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko kwa kukutana na kuzungumza na wajumbe wa mkutano, hapo tarehe 15 Juni 2015.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.