2015-06-12 17:15:00

Chuchumilieni utakatifu wa maisha kwa kujikita katika mchakato wa Uinjilishaji


Mapadre katika maisha na utume wao wanapaswa kwa namna ya pekee kuhakikisha kwamba, wanachuchumilia utakatifu wa maisha pamoja na kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji, utume unaovaliwa njuga na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Ni changamoto ambayo imetolewa na Padre Raniero Cantalamessa, mhubiri wa nyumba ya kipapa, wakati wa tafakari kwenye mafungo ya kiroho ya wakleri kimataifa, yanayoendelea kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano hapa mjini Roma.

Haya ni mafungo ambayo yameandaliwa na Chama cha Kitume cha uhamsho kimataifa kwa kushirikiana na Chama cha udugu wa Kikatoliki, lengo ni kuchuchumilia utakatifu wa maisha kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji mpya unaofumbata Injili ya Furaha, chemchemi ya furaha na matumaini mapya, pale waamini wanapobahatika kukutana na Yesu Kristo. Hii ni furaha kwa ajili ya wote na wala si kwa ajili ya wateule wachache wanaoweza kuigharamia wenyewe, bali ni furaha kwa wote, lakini zaidi kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Padre Cantalamessa anabainisha kwamba, wimbo bora zaidi unaobubujika furaha ya kweli ni ule ulioimbwa na Bikira Maria yaani “Magnificat”, unaoelezea jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo anavyowanyanyua na kuwakweza wanyonge na maskini na kuwatweza wenye kiburi. Hii ni changamoto kwa Mapadre ambao wako karibu sana na Chama cha Uhamsho wa Kikristo kuhakikisha kwamba, wanatumia karama na mapaji ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa na wala si vinginevyo. Wajitahidi kukita maisha yao katika Kristo na Roho Mtakatifu.

Wakleri kwa namna ya pekee kabisa wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanakumbatia na kuchuchumilia utakatifu wa maisha, kipimo makini cha ufanisi wa shughuli na mikakati ya kichungaji katika mchakato wa Uinjilishaji mpya. Hii ni dhamana nyeti katika maisha na utume wa Wakleri, ili kuwaonesha watu njia inayowaongoza kwenda kwa Kristo.

Wakleri watoe maamuzi kila mmoja kadiri ya dhamiri yake nyofu, ikiwa kama anataka kuwa ni dira na mwanga kwa ndugu zake katika Kristo, ili waweze kuiona njia inayowaelekeza kwa Kristo Yesu au wanataka kuwa ni vikwazo na magogo yanayowaangisha waamini katika hija ya maisha yao ya kiroho! Hapa Wakleri wanapaswa kuchagua, kusuka au kunyoa! Vinginevyo, siku moja watashikwa na bumbuwazi katika maisha na utume wao!

Kwa upande wake, Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani, katika tafakari yake kwenye mafungo haya, amekazia kwa namna ya pekee, upendo ule wa dhati ambao Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuuzungumzia mara kwa mara katika mahubiri yake, siku ile Wakleri waliposikia wito na kukutana na Yesu kwa mara ya kwanza katika hija ya maisha yao, kiasi cha kuwaachia chapa ya kudumu wanayopaswa kuipyaisha kila kukicha.

Kardinali Turkson anasema kwamba, kutokana na udhaifu wa binadamu, Wakleri wanaweza kujikuta wamebwagwa chini kama ilivyotokea kwa Mitume wa Yesu, kusambaratika kila mtu kivyake vyake, lakini baada ya ufufuko wa Kristo, akawaimarisha katika maisha na utume wao, wakawa tayari kujisadaka kwa ajili ya kuwatangazia Watu wa Mataifa Injili ya Furaha.

Hali hii inahitaji fadhila ya unyenyekevu, imani na matumaini makuu, ili kuthubutu kumfungulia Yesu malango ya mioyo na maisha yao, ili aweze kuwakirimia toba, msamaha na upatanisho; mambo msingi yanayoweza kuwasadia Wakleri kufurahia tena wito na maisha yao ya Kipadre. Mafungo haya bado yanaendelea hapa mjini Vatican kwa tafakari kutoka kwa viongozi mbali mbali wa Kanisa kutoka mjini Vatican.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, itaendelea kukushirikisha kwa muhtasari yale yanayojiri katika mafungo haya ya Wakleri kimataifa, ili kuweza kuchuchumilia utakatifu wa maisha kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.