2015-06-11 15:25:00

Yaliyojiri katika mkutano wa Baraza la Makardinali washauri!


Mkutano wa kumi wa Baraza la Makardinali Washauri wa Baba Mtakatifu ulioanza hapo tarehe 8 Juni umehitimishwa, Jumatano tarehe 10 Juni 2015. Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, pamoja na mambo mengine muhimu, Makardinali chini ya uongozi wa Baba Mtakatifu Francisko wamejadili kuhusu mabadiliko katika sekta ya uchumi na fedha; mchakato wa kuwalinda watoto wadogo pamoja na uratibishaji mpya wa vyombo vya mawasiliano vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican.

Makardinali katika mkutano huu wameamua kuanzisha mahakama maalum itakayojihusisha na mchakato wa kulinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso na dhuluma. Mahakama hii itashughulikia kesi za Maaskofu ambao wameshindwa kuwajibika barabara katika kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia. Lengo ni kuhakikisha kwamba, vitendo hivi vya aibu havijirudii tena ndani ya Kanisa.

Makardinali pia wameendelea kutafakari kuhusu muswada wa marekebisho ya Sekretarieti kuu ya Vatican ambao utaendelea kuboreshwa zaidi ili kuzaa matunda yanayokusudiwa. Kardinali George Pell, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya uchumi amefafanua kuhusu mchakato wa mabadiliko unaoendelea kwa sasa kadiri ya katiba ya Sekretarieti ya uchumi. Kuna vitendo vikuu vitatu vinavyotarajiwa kuanzishwa: cha kwanza kitashughulikia upembuzi yakinifu wa mapato ya Vatican na vitega uchumi; cha pili kitashughulikia rasilimali watu na kitengo cha tatu kitajikita katika masuala ya mfumo wa mawasiliano uliopo kwa sasa.

Kardinali Sean Patrick O’Malley amefafanua dhamana ya Tume ya kulinda watoto wadogo baadaye kufuatiwa na majadiliano ya kina na Baba Mtakatifu Francisko akaridhia uamuzi kwamba, kwa Maaskofu watakaoshindwea kuwajibika kwenye kesi za nyanyaso dhidi ya watoto wadogo zitapaswa kupelekwa kwenye Baraza la Kipapa la Maaskofu, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu pamoja na Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki.

Baba Mtakatifu atatoa mamlaka kwa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kutoa maamuzi kwa kesi za nyanyaso za kijinsia na kwamba, hapa kutaanzishwa Mahakama maalum na itakuwa na Katibu wake atakayeshughulikia masuala ya sheria, mahakama na haki. Ufanisi wa kitengo hiki utakuwa unapimwa kila baada ya miaka mitano.

Makardinali wamejadili taarifa ya vyombo vya upashanaji habari vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican kama ilivyowasilishwa kwao na Monsinyo Dario Viganò, Mkurugenzi mkuu wa Kituo cha Televisheni cha Vatican, CTV, aliyeteuliwa hivi karibuni kusimamia Tume ya Marekebisho ya vyombo vya habari vya Vatican. Makardinali wapewa muswada wa marekebisho unaopaswa kufanyiwa kazi katika kipindi cha miaka minne kuanzia sasa, kwa kushirikishana rasilimali watu, wakati Baraza jipya litakapokuwa limeundwa.

Baraza la Kipapa la haki na amani, limewasilisha mapendekezo mbele ya Baraza la Makardinali kuhusiana na Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko kuhusu mazingira, unaotarajiwa kuzinduliwa rasmi hapo tarehe 18 Juni 2015. Ili kuweza kupata ushiriki mpana zaidi kutoka kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, kushirikisha mawazo na mapendekezo yao, ili kwamba, Waraka huu uweze kuchukuliwa kuwa ni dhamana na Kanisa zima katika mchakato wa kulinda na kutunza mazingira.

Ufafanuzi huu umetolwa na Padre Michael Czerny kutoka Baraza la Kipapa la haki na amani. Baraza la Makardinali Washauri, litakutana tena kuanzia tarehe 14 hadi 16 Septemba 2015.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.