2015-06-11 16:19:00

Wakristo wanachangamotishwa kutembea, kuhudumia na kujisadaka!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Alhamisi, tarehe 11 Juni 2015, Kumbu kumbu ya Mtakatifu Barnabas mtume, amekazia mambo makuu matatu yanayopaswa kutekelezwa na waamini; yaani: kutembea, kuhudumia na kujisadaka, ili kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa kushinda kishawishi cha kudhani kwamba, wokovu unaweza kupatikana kwa njia ya utajiri.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Yesu aliwatuma wafuasi wake kwenda duniani kote ili kutangaza Habari Njema ya Wokovu, ili kuwapatia watu Neno la Uzima linaliowajalia wokovu. Utume huu si matembezi ya hiyari anasema Baba Mtakatifu, kwani huu ni utekelezaji wa dhama ambayo Wakristo walijitwalia wakati walipopokea Sakramenti ya Ubatizo.

Maisha ya Mkristo wa kweli yanaambata ari na utume wa kimissionari, kwa kutoka katika ubinafsi na makando kando yake, tayari kushiriki katika dhamana hii nyeti inayomwajibisha katika sala, tafakari na maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Mkristo aliyeshibana na Yesu anauhakika wa kufanikisha mchakato wa Uinjilishaji vinginevyo, anajisumbua bure, kwani Injili itakosa nguvu, mvuto na mashiko.

Mkristo asiyethubutu kuhudumia kwa hakika anapoteza dira na mwelekeo wa maisha. Wakristo wawe ni watu wanaofanya hija kwa ajili ya kuhudumia, huku wakijikita katika mafundisho makuu ya Yesu ambayo muhtasari wake unapatikana katika Heri za Mlimani. Hii ndiyo dira inayopasa kuwaongoza wakristo katika maisha na utume wao. Maisha ya Kikristo ni kwa ajili ya huduma na kamwe wakristo wasimezwe na ubinafsi, bali wajitoe kimasomaso kwa ajili ya utume na maisha ya Kanisa bila kutafuta utajiri wala kumezwa na malimwengu. Yesu Kristo awe ni mfano na kielelezo cha sadaka na huduma kwa watu wake, kwa kutambua kwamba, anawapatia matumaini ambayo kamwe hayawezi kudanganya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.