2015-06-11 15:40:00

Rais Vladimir Putin akutana na kuzungumza na Papa Francisko mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi jioni tarehe 10 Juni 2015 amekutana na kuzungumza na Rais Vladimir Putin wa Russia, mazungumzo ambayo yamedumu kwa takribani dakika 50, baadaye viongozi hawa wawili wamebadilishana zawadi. Baba Mtakatifu amempatia Rais Putin medali ya msanii Guido Veroi inayomwonesha Malaika wa amani, mwaliko wa kujenga mshikamano na amani duniani kwa  kujikita katika haki pamoja na nakala ya Waraka wake wa kichungaji Injili ya Furaha, Evangelii gaudium.

Katika taarifa iliyotolewa na Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, mazungumzo kati ya viongozi hawa wawili yamejikita zaidi katika masuala ya kimataifa, lakini kwa namna ya pekee, hali tete inayoendelea kujitokeza nchini Ukraine na huko Mashariki ya Kati. Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa kujikita katika mchakato wa kutafuta suluhu ya kudumu huko Ukraine kwa kuzingatia ukweli na uwazi, ili amani iweze kupatikana. Hapa kuna haja ya kujenga utamaduni wa majadiliano na kwamba, pande zote zinazohusika zijitahidi kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa mjini Minsk.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, kwa sasa kuna haja ya kushughulikia kwa ukamilifu zaidi mahangaiko ya watu wa Ukraine, kwa kutoa nafasi kwa watoa misaada wa kimataifa kuweza kuwasaidia watu wanaoendelea kuteseka, ili taratibu amani na utulivu viweze kurejea tena katika Ukanda huu. Kuhusiana na mgogoro wa kivita unaoendelea huko Mashariki ya Kati, Syria na Iraq; viongozi hawa kimsingi, wameafiki mambo msingi waliyokuwa wamekwisha kubaliana kuhusiana na mchakato wa amani unaopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa. Watu wanaoishi huko Mashariki ya Kati wanapaswa kuhakikishiwa usalama wa maisha yao, bila kusahau waamini wa dini mbali mbali huko Mashariki ya kati, lakini kwa namna ya pekee Wakristo.

Padre Lombardi anafafanua kwamba, wakati Baba Mtakatifu Francisko alipokuwa anafanya mkutano na Rais Putin, Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican, amefanya mkutano pia na  Bwana Sergey Lavrov, Waziri wa mambo ya nchi za nje nchini Russia. Viongozi hawa wamezungumzia pia mgogoro wa kivita huko Mashariki ya Kati na Ukraine.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.