2015-06-10 11:12:00

Waamini 800 wapokea Ekaristi Takatifu kwa mara ya kwanza Jimbo kuu la Dodoma


Ekaristi Takatifu ni fumbo la upendo linalowakutanisha waamini na Yesu Kristo katika hija ya maisha yao ya kiroho, tayari kuwashibisha kwa chakula na kinywaji kilichoshuka kutoka mbinguni, kwa ajili ya maisha ya uzima wa milele. Katika Sakramenti hii, Yesu anawaonjesha upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Ili waamini waweze kuliishi kikamilifu Fumbo la Ekaristi Takatifu wanapaswa kushiriki kwa ibada na uchaji maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu; kukuza na kudumisha Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, tayari kumwilisha Ibada hii katika huduma ya upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Yesu Kristo, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, anawavuta watu wote kwake katika mapendo na hii ndiyo dhana ya Fumbo la Ekaristi inayotoa mwelekeo wa mapendo kamili kwa Mungu na jirani.

Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu ni chemchemi na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ni sadaka na uwepo endelevu wa Yesu Kristo kati ya wafuasi wake, mwaliko na changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanashiriki kwa ukamilifu maadhimisho yote ya Ibada ya Misa Takatifu kwa uchaji na ufahamu, ili kupata neema na baraka zinazotolewa na Mama Kanisa katika adhimisho hili.

Huu ni mwaliko ambao umetolewa na Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo kuu la Dodoma katika maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu yaliyofanyika kwenye Kituo cha Hija cha Mbwanga, Jimbo kuu la Dodoma na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa Familia ya Mungu, Jimbo kuu la Dodoma. Katika Ibada hii ya Misa Takatifu, wakristo 800 wamepokea Komunio ya kwanza.

Waamini wanahimizwa kuhakikisha kwamba, wanajiandaa barabara kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, ili kumpokea Yesu katika Ekaristi Takatifu, ili aweze kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo; kielelezo cha afya bora ya maisha ya kiroho. Wakristo waliopokea Ekaristi Takatifu kwa mara ya kwanza katika maisha yao, wanaendelea kuhimizwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanashiriki mara kwa mara katika Karamu ya Bwana, tayari kuwakirimia nguvu na ari ya kumshuhudia Kristo kama kielelezo cha imani inayomwilishwa katika matendo.

Wakati huo huo, Askofu mkuu Beatus Kinyaiya anayetarajiwa kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kupatiwa Pallio Takatifu, Kanisa litakapokuwa linaadhimisha Siku kuu ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume, hapo tarehe 29 Juni 2015 anawaalika waamini wa Jimbo kuu la Dodoma, kujiandaa kwa ajili ya kumpokea na kumkarimu, Askofu mkuu Francisco Padilla, Balozi wa Vatican nchini Tanzania, takayefika Jimbo kuu la Dodoma, Juma la pili la Mwezi Julai, ili kumvisha Askofu mkuu Beatus Kinyaiya, Pallio Takatifu atakayokuwa amepewa na Baba Mtakatifu Francisko.

Itakumbukwa kwamba, kuanzia sasa Maaskofu wakuu watakuwa wanavishwa Pallio Takatifu na Mabalozi wa Vatican kwenye nchi husika, ili kutoa nafasi kwa Familia ya Mungu inayounda Jimbo kuu, kushiriki kikanilifu katika maisha na utume wa Kanisa mahalia. Askofu mkuu Beatus Kinyaiya aliyeteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko anakuwa ni Askofu mkuu wa kwanza wa Jimbo kuu la Dodoma kuanza kutekeleza agizo lililotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kuhusiana na Pallio Takatifu.

 

Na Rodrick Minja

Dodoma, Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.