2015-06-10 07:50:00

Uzalishaji wa mazao ya chakula hauna budi kukabiliana na changamoto zilizopo


Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuhakikisha kwamba, inabadili mbinu za uzalishaji wa chakula, ili kuweza kuweka uwiano na muunganiko mzuri kati ya mchakato wa uzalishaji wa chakula na utunzaji bora wa mazingira. Wadau mbali mbali katika sekta ya kilimo na uzalishaji wa mazao ya kilimo, hawana budi kufikiri na kutenda ili kulinda na kutunza mazingira, kwa ajili ya kizazi cha sasa na kile kijacho. Uzalishaji wa mazao ya chakula hauna budi kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Ikumbukwe kwamba, idadi ya watu inaendelea kuongezeka kila mwaka, kumbe, sekta ya kilimo inapaswa kuwa na mbinu pamoja na mikakati ya kuzalisha chakula bora na cha kutosha kwa ajili ya matumizi ya mwanadamu. Hii ni changamoto ambayo imetolewa hivi karibuni na Dr. Graziano da Silva, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kilim ona Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kwa mwaka 2015, iliyoadhimishwa kimataifa, huko Milano, Kaskazini mwa Italia.

Sekta ya kilimo ina dhamana ya kuzalisha chakula kwa watu zaidi ya billioni mbili ifikapo mwaka 2050. Tatizo kubwa linalosababisha baa la njaa duniani ni kutokana na watu kutokuwa na uwezo wa kupata chakula, ambacho kimsingi kipo na kinaweza kutosheleza mahitaji ya watu wote duniani. Kwa bahati mbaya, familia maskini hazina nguvu ya kiuchumi ya kununua chakula ambacho kweli wanakihitaji. Hii ni changamoto kubwa kwa FAO ambayo imekuwa inafanyiwa kazi tangu baada ya Vita kuu ya Pili ya Dunia.

Sera na mikakati makini ya uzalishaji wa mazao ya chakula ni muhimu sana katika kupambana na baa la njaa na lishe duni duniani sanjari na utunzaji bora wa mazingira. FAO inakadiria kwamba, kila mwaka kuna tani millioni 222 za chakula kinachotupwa, ambacho kingeweza kutumiwa na watu sehemu mbali mbali za dunia.

FAO inabainisha kwamba athari za mabadiliko ya tabianchi ni kati ya changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa katika harakati za kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na uhakika wa usalama wa chakula duniani. Mkutano wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika mjini Paris,Ufaransa, Desemba 2015, itakuwa ni fursa makini kwa Jumuiya ya Kimataifa kupanga mikakati na sera zinazotekelezeka kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kuna haja pia ya kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na usambazaji bora wa chakula duniani, ili kupambana na baa la njaa na utapiamlo. Uzalishaji wa mazao ya chakula hauna budi pia kuratibiwa na sera na mikakati ya teknolojia mpya, rafiki kwa mazingira, ili kupunguza uzalishaji mkubwa wa hewa ya ukaa. Chakula kwa wote ndiyo dira na mwongozo katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.