2015-06-10 15:32:00

Siku kuu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, Siku ya kuombea Utakatifu wa Mapadre


Wapendwa taifa la Mungu, Utukuzwe Moyo Mtakatifu wa Yesu! Leo Mama Kanisa, anasherehekea Sikukuu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, Moyo uliochomwa mkuki pale Msalabani sanjari na Siku ya Kimataifa kwa ajili ya kuombea Utakatifu wa Mapadre. Kumbe Mama Kanisa anasherehekea chemchemi ya neema za Mungu. Sherehe hii ni kati ya sherehe za Bwana kadiri ya mpango wa kilitrujia ambayo huja kila Ijumaa ya pili baada ya sherehe ya Pentekoste.

Mara moja tunaposikia neno Moyo Mtakatifu wa Yesu, tunapaswa kukumbuka maneno ya Mt Yohane, asemaye “tazama jinsi Mungu alivyoupenda ulimwengu”. Na hivi bila kubabaika tunatambua kuwa ni mapendo ya Mungu kwa wanadamu wote na kwa vizazi vyote. Kanisa likitafakari zawadi hiyo kubwa ya mapendo ya Mungu kwa wanadamu wote, haliachi kutumia zawadi hiyo kusogeza karibu neema za Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa mapadre wake, ndiyo kusema leo pia ni sikukuu ya kutakatifuzwa kwa mapadre.

Majitoleo kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu si jambo la leo, ni jambo ambalo limekuwepo tangu mwanzo wa Kanisa. Papa Alexander I aliwahi kufundisha kuwa Kanisa limezaliwa toka mateso ya Kristo na hasa pale anapochomwa mkuki ubavuni mwake na hivi yakatoka Damu na maji, Damu chemchemi ya ukombozi wetu, Damu mto wa rehema kwa watu wote. Mtakatifu Yustino katika karne ya II yeye anasema sisi ni Israeli mpya tuliozaliwa toka Moyo Mtakatifu kama maji yatokayo mwambani. Mt. Ireneo wa Lyonsi katika karne ya III yeye anasema kuwa Kanisa ni kile kisima cha maji ya uhai yanayobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu.

Katika majitoleo kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, Mama Kanisa atualika kila Sikukuu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu kushiriki Misa Takatifu, kupokea Ekaristi Takatifu na kutenda matendo ya huruma, kusali sala iliyoelekezwa na Mama Kanisa kama njia ya kulipia madhulumu dhidi ya Moyo Mtakatifu wa Yesu yafanywayo na watu mbalimbali na hasa kwa kukosa heshima kwa Sakramenti Kuu, yaani Ekaristi Takatifu. Matunda ya majitoleo hayo ni neema zibubujikazo toka Moyo Mtakatifu wa Bwana.

Wapendwa taifa takatifu, tukiwa na nia njema tumfuase Bwana tukitafakari Neno lake ambalo Mama Kanisa ametuwekea leo hii katika Sikukuu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Katika somo la kwanza Mungu anaongea na Waisraeli kwa njia ya Nabii Hosea. Anawaambia jinsi alivyowapenda, akisema walipokuwa wadogo aliwatoa utumwani Misri na kuwaongoza polepole pasipo hasira mpaka nchi ya ahadi. Katika safari kunajitokeza ukaidi lakini katika Moyo wake daima kuliwaka huruma na mapendo yasiyokwisha. Anaahidi hawezi kuangamiza taifa lake tena. Mafundisho haya ni kiashirio tosha cha mapendo yake kwetu sisi tulio taifa jipya la Israeli lililozaliwa toka chemchemi ya mapendo ya Moyo wake. Ndiyo kusema basi tunaalikwa kujiweka wakfu katika Moyo Mtakatifu wa Yesu il bubujiko la mapendo upeo lizame katika familia na Jumuiya zetu, tukijitahidi kusali kwa ajili ya kulipia dhambi zetu na adhabu zake.

Mwinjili Yohane anatupatia mafundisho juu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu akisimulia tukio la kuchomwa ubavu wa Kristo kwa mkuki pasipo huruma na kutoka Damu na maji. Ni katika tendo hili kama tulivyokwisha sema hapo mwanzoni kunazaliwa Kanisa, chombo cha huruma ya Mungu, mwalimu wa mataifa na safina safi ya kuwapeleka watu mbinguni. Ni katika tendo hilo ambalo linagusa Moyo wa Bwana kunazaliwa huruma upeo, ambayo inaondoa mipaka, inasamehe pasipo hasira, inaita kila mmoja wetu kwa ajili ya kuteka maji katika kisima cha wokovu. Ndiyo kusema Moyo Mtakatifu wa Yesu ni safina ya mapumziko kwa wale wanaosumbuka na kulemewa na mizigo kama tusomavyo katika Injili ya Matayo 11: 25-30.

Mtakatifu Paulo anapowaandikia Waefeso anaanza kwa kusema kuwa kila alichonacho ni kwa neema tu. Maana katika udogo wake amepata kukirimiwa neema na uwezo wa kutangaza habari njema kwa mataifa. Habari hii njema ni utajiri wa Mungu usiopimika ambao unatangazwa na Mama Kanisa, Kanisa ambalo limezaliwa toka mateso na ufufuko wa Bwana. Kanisa ambalo ni chemchemi ya maji yale yabubujikayo toka Moyo wa Bwana. Ni katika utajiri huo, Mt. Paulo anamwalika kila mmoja wetu apige goti kwa Baba wa mbinguni kupitia Moyo Mtakatifu wa Yesu.

Goti hili litakuwa la maana likiwa limejikita katika upendo ambao twauchota katika Moyo uleule usioisha wala kupungua uzuri wake wa Kimungu, uzuri unaovuka kipimo cha upeo wetu. Mt. Paulo anasonga mbele akitualika kuendelea katika kumtukuza Kristo Yesu ambaye alitupenda mapendo upeo, mapendo ambayo lazima tuyaweke katika maisha yetu ya kila siku.

Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika ule Waraka wa kichungaji juu ya Kanisa katika ulimwengu "Gaudium et Spes" unawaalika waamini kuitazama dunia katika mtazamo chanya na kuweka chachu ya Injili kama Kristu alivyoweka chachu ya mapendo kwa njia ya umwilisho wake. Kwa sababu hiyo pia, Leo kanisa linasali kwa kuuelekea Moyo Mtakatifu wa Yesu ili mapendo ya moyo huo yakae ndani ya ulimwengu na ulimwengu huu uwe ni mahali pema pa kuishi.

Baada ya tafakari toka Neno la Mungu naomba tuchukue maneno machache katika lugha yetu ya kila siku yatusaidie katika kutambua mwelekeo wa mwanadamu kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Daima Nasikia watu wakisema "Jamaa yule ana moyo" na labda nawe umesikia! Unalo swali juu ya hili? Mimi nina swali “ mbona watu wote wana mioyo? Kwa vyovyote vile hapa kuna jambo la ziada ambalo haligusiki, natumai si moyo wa nyama bali moyo wa mahusiano mema na watu wengine na hivi moyo wa mapendo ya kimungu. Katika kuendelea kufuatilia nimesikia pia watu wakisema "jamaa yule ana moyo mkuu" ndiyo kusema anao moyo wa kustahimili, kutafakari na kuvumilia mateso yampatayo katika maisha yake. Basi mpendwa unayenisikiliza ebu chukua nafasi kidogo ujiulize kwa upole na unyenyekevu, je mimi ninao moyo gani?

Mpendwa msikilizaji ni katika dodoso kama hiyo nimesikia pia watu wakisema "jamaa yule ana moyo mpole" kwa jinsi hiyo jamaa huyu anao moyo wa mapendo yatokayo katika Moyo Mtakatifu wa Yesu, maana Bwana mwenyewe amesema "mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo”.

Wapendwa, tokana na tafakari hii, kama mmoja atakuuliza nini maana ya Sikukuu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, mara moja sema sikukuu ya Mapendo ya Mungu yasiyopimika, mapendo ya Mungu yasiyofahamu hasira bali huruma isiyo na upeo ambayo kila mmoja wetu hata angekuwa na dhambi kiasi gani anaalikwa kuja na kumwangukia Bwana asemaye njooni kwangu ninyi mnaoelemewa na kusumbuka na mizigo nitawapumzisha.

Mama Kanisa amechagua Sikukuu hii iwe ni kwa ajili ya kuwatakatifuza mapadre ili wajazwe neema na baraka tele kwa ajili ya kazi yao ya kichungaji inayodai mapendo ya kimungu. Si tu kwa ajili ya kuwatakatifuza mapadre bali ni pia kwa ajili ya taifa zima la Mungu ambalo linahitaji upendo na hasa wakati huu wa machafuko sintofahamu! Kumbe, ni sikukuu ya kutakatifuzwa kwa waamini wote, maana mapadre si kwa ajili yao wenyewe bali kwa ajili ya uchungaji uliojazwa nguvu ya Kimungu. Wanatakatifuzwa ili waweze kukaa katika kifua cha Bwana na wavumilie utume wao mpaka wanapofikisha taifa la Mungu katika Yerusalem mpya. Wanatakatifuzwa ili maisha yao yawe ni chachu kwa maisha ya watu, yawe ni Ekaristi,  mkate umegwao katika jumuiya kama asemavyo Mtakatifu Ursula.

Tunaalikwa basi leo kuwaombea mapadre wote na Wanaushirika wa Moyo Mtakatifu wa Yesu ulimwenguni ili maisha yao yawe changamoto kwa taifa zima la Mungu. Tunawatakieni heri na Baraka tele zitokazo katika Moyo Mtakatifu wa Bwana wetu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.