2015-06-10 12:14:00

Msiwe na kishawishi cha kutaka kubaki matawi ya juu ili kula kuku kwa mrija!


Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanabainisha kwamba, kati ya fadhila zinazohitajika zaidi kwa huduma ya Mapadre, inawabidi ukumbukwe ule moyo ambao unawafanya wawe tayari kila wakati kutafuta siyo mapenzi yao binafsi, bali mapenzi ya yule aliyewatuma. Hii ni dhamana inayotekelezwa ndani ya Kanisa kwa njia ya umoja na mshikamano. Mapadre waoneshe moyo wa utii na unyenyekevu kwa dhamana na majukumu wanayokabidhiwa na Mama Kanisa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu katika ujumla wake.

Hivi karibuni, Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu Mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu ambaye pia ni Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa, aliwashukuru na kuwapongeza wanafunzi mbali mbali waliohitimu masomo yao kutoka katika vyuo vikuu vya kipapa na sasa wanajiandaa kurejea kwenye Makanisa mahalia, tayari kushirikisha ujuzi, maarifa na hekima waliyojichotea wakati wa majiundo yao hapa Roma.

Katika hafla hiyo, Askofu mkuu Rugambwa amewapongeza wanafunzi kutoka Tanzania waliotumwa na Maaskofu pamoja na wakuu wao wa Mashirika kwa kuonesha bidii, majitoleo, ari na sadaka ya kumaliza masomo, ili waweze kurejea tena nchini Tanzania kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, kwa ari na nguvu mpya zaidi baada ya kuhitimu masomo yao.

Kama wanafunzi wanakabiliwa na changamoto nyingi katika masomo yao, lakini wengi wao wamejitahidi kuvuka vikwazo na changamoto hizi na hatimaye, kuhitimu masomo yao na sasa wanajiandaa kurejea nchini Tanzania, jambo linalotia moyo! Mkazo unaotolewa na viongozi wa Kanisa kwa Mapadre, Watawa na Majandokasisi waliohitimu masomo yao ni kuhakikisha kwamba, wanarejea makwao, tayari kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina na kamwe wasiwe na kishawishi cha kutaka kubaki “matawi ya juu na kuendelea kula kuku kwa mrija”. Wanafunzi wanapohitimu masomo yao, wawe wepesi kurejea nchini mwao anasema Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.