2015-06-10 10:45:00

Familia ni hospitali ya kwanza iliyo karibu zaidi na wagonjwa!


Magonjwa ndani ya familia ndiyo mada iliyoongoza Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko kwa mahujaji na wageni waliokuwa wamefurika mjini Vatican siku ya Jumatano tarehe 10 Juni 2015. Ugonjwa ni sehemu ya mang’amuzi ya binadamu tangu mtoto anapozaliwa, lakini zaidi anapokuwa mzee. Familia inakuwa ni mahali ambapo wanafamilia wanaonjeshana upendo wa dhati, hata pale inapokuwa ni vigumu kwa wazazi kuweza kukubali mateso na mahangaiko ya watoto wao wagonjwa.

Familia anasema Baba Mtakatifu, tangu mwanzo imekuwa ni hospitali iliyo karibu zaidi na wagonjwa. Leo hii mgonjwa kulazwa hospitalini inaonekana kana kwamba, ni upendeleo wa watu wachache na pengine hospitali yenyewe inaweza kuwa iko mbali. Wanafamilia wenyewe ndio wanaojipanga barabara kwa ajili ya kutoa huduma makini kwa mgonjwa wao na kumsaidia ili aweze kupona.

Baba Mtakatifu anaendelea kubainisha kwamba, katika Maandiko Matakatifu, Yesu alibahatika kukutana na hatimaye kuwaponya wagonjwa. Uponyaji kilikuwa ni kiini cha maisha na utume wa Yesu, kiasi kwamba, wakati mwingine alishutumiwa kwa kuvunja Sheria, lakini upendo wa Yesu ulikuwa ni mkubwa zaidi kuliko hata Sheria. Aliwataka wafuasi wake kuendeleza dhamana na utume huu, kwa kuwapatia nguvu ya kuponya, kwa kugusa madonda yao ya ndani, ili kuwarimia amani na uponyaji.

Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, ugonjwa wa mwanafamilia unaweza kuwa ni changamoto kubwa kwa wanafamilia wengine. Kama wafuasi wa Kristo, waamini kwa namna ya pekee, wanaalikwa kusali bila kukoma kwa ajili ya wagonjwa na watu ambao wako kufani pamoja na kuzisaidia familia zinazokabiliwa na changamoto ya ugonjwa.

Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanahamaishwa kuwafundisha watoto wao moyo wa upendo na mshikamano kwa wagonjwa, ili wasiwe baridi na wagumu kwa mateso na mahangaiko ya wengine, bali watu wenye uwezo wa kuwasaidia wagonjwa na kuishi kwa ukamilifu ubinadamu wao. Baba Mtakatifu anawaalika Wakristo kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Kanisa ambalo linaendelea kujisadaka kwa njia ya huduma kwa familia wakati wa kuuguliwa na kati ya familia zenyewe.

Baba Mtakatifu anaendelea kusali kwa ajili ya kuwaombea wagonjwa ili waweze kuimarika katika imani yao, tayari kuwa ni mashuhuda matumaini na mapendo. Pale wanapokumbana na mitikisiko ya maisha ya kiroho, wasisahau kukimbilia hifadhi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu anayeweza kuwakirimia amani na utulivu wa ndani. Ugonjwa unaweza pia kuwa ni nafasi ya kupokea neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu na chemchemi inayoimaarisha hekima moyoni. Waamini wawe karibu na watu wanaouguliwa ndani ya familia. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru na kuwapongeza watawa wa Mashirika mbali mbali waliokuwepo kwenye Katekesi yake siku ya jumatano, kwa kuwataka kuwaonesha watu uso wa huruma na upendo wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.