2015-06-10 08:17:00

Elimu ni chombo cha huduma na majadiliano kwa ajili ya ustawi na maendeleo


Dhamana ya kuelimisha leo na kesho ndiyo kauli mbiu iliyofanyiwa kazi na wajumbe walioshiriki katika Jukwaa la majadiliano lililoandaliwa na Askofu mkuu Francesco Follo, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO, wakati huu Shirika hili linapofanya kumbu kumbu ya miaka 70 tangu lilipoanzishwa. Majadiliano haya yamefanyika, hivi karibuni kwenye Makao makuu ya UNESCO mjini Paris, Ufaransa, kwa kuwashirikisha wadau mbali mbali kutoka katika sekta ya elimu.

Hapa elimu inachukuliwa kama chombo cha kukoleza mchakato wa maendeleo endelevu ya mwanadamu katika medani mbali mbali za maisha pamoja na kukoleza majadiliano ya kitamaduni, ili watu waweze kufahamiana, kueshimiana na kuishi kwa amani, umoja, upendo na mshikamano. Mama Kanisa pia anafanya kumbu kumbu ya Jubilei ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Tamko juu ya Elimu ya Kikristo, lijulikanalo kama “Gravissimum Educationis.

Tamko hili pamoja na mambo mengine linakazia dhamana ya elimu, haki ya watu kupata elimu, maana ya elimu; elimu ya Kikristo; wenye dhamana na wajibu wa kutoa elimu, taratibu za elimu ya Kikristo; Umuhimu wa shule, wajibu na haki za wazazi; umuhimu wa elimu ya kimaadili na kidini shuleni; shule zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki; aina mbali mbali za shule za Kikatoliki; Vitivo na Vyuo vikuu vya Kikatoliki; vyuo vya kitaalimungu kwa ajili ya majiundo ya mapadre na watawa.

Mama Kanisa anaadhimisha pia Jubilei ya Miaka 25 tangu Papa Yohane Paulo II alipochapisha Katiba ya Kitume ya Vyuo vikuu vya Kikatoliki inayojulikana kwa lugha ya Kilatini kama Ex corde ecclesiae, iliyotolewa kunako mwaka 1990, kama sehemu y amchango wa Kanisa katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayojikita katika misingi ya haki, amani na utulivu; kwa kukazia ukweli, asili, mtu na uwepo wa Mungu. Lengo ni kukuza na kudumisha uhuru, haki na utu wa mtu.

Kanisa linataka kusaidia mchakato wa maboresho ya sekta ya elimu inayojikita katika huduma kwa jamii kwani linatambua matatizo na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika sekta ya elimu kwa vijana wa kizazi kipya. Kumbe, miaka 70 ya UNESCO, Miaka 50 ya Tamko la Dhamana ya Elimu“Gravissimum Educationis” na Miaka 25 ya Katiba ya Vyuo vikuu vya Kikatoliki ni fursa makini ya kuangalia changamoto zilizoko mbele ya Jumuiya ya Kimataifa.

Kardinali Zenon Grocholewski, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki anabainisha kwamba, UNESCO iliundwa baada ya Vita kuu ya Pili ya Dunia. Jumuiya ya Kimataifa ilikuwa na kiu ya kuona haki na amani vinatawala tena katika mioyo na akili za watu sanjari na kujenga umoja na mshikamano wa kimataifa kwa ajili ya mafao ya wengi. Elimu ikaonekana kuwa ni chombo ambacho kingeweza kuwasaidia watu kukumbatia mafao ya wengi. Ili Jamii iweze kutekeleza dhamana na wajibu huu nyeti kuna haja ya kuwa na walezi waliofundwa wakafundika; watu wanaothamini wito na kazi zao, tayari kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya vijana wa kizazi kipya. Mafanikio ya elimu ni matokeo ya jitihada, ujuzi, maarifa, sadaka, mbinu na teknolojia katika ufundishaji na urithishaji wa elimu, ujuzi na maarifa.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika hotuba yake kwenye majadiliano haya anapembua kwa kina na mapana mchango wa Kanisa katika sekta ya elimu kwa kukazia uchumi unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu. Kanisa ni muasisi wa mchakato wa elimu na hii imekuwa ni sehemu ya maisha na utume wake katika mchakato wa Uinjilishaji unaopania kumletea mwanadamu ukombozi kamili.

Maendeleo ya sayansi na teknolojia yasaidie mchakato wa maboresho katika elimu kama wanavyobainisha Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu. Elimu haina budi kuwa ni chombo cha majadiliano ya kitamaduni, ili kujenga na kudumisha utamaduni wa haki, amani na mapendo ya kweli.

Sekta ya elimu inakabiliwa na changamoto mbali mbali kati ya changamoto hizi anasema Kardinali Parolin ni umuhimu wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu, jambo ambalo kwa sasa linapuuzwa kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia . Kanuni maadili na tunu msingi za maisha ya kiutu na kiroho hazina nafasi tena. Mchango wa familia na Kanisa katika elimu hauna thamani tena, matokeo yake ni kukua na kushamiri kwa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu. Ubinafsi na uhuru usiokuwa na mipaka ni matokeo ya changamoto hii.

Changamoto ya pili anasema Kardinali Parolin, ni kumong’onyoka kwa tunu msingi za kimaadili, kiutu na maisha ya kiroho, kiasi kwamba, mchakato wa elimu unayumba kwa kukosa msingi thabiti ambao unapaswa kujengwa tangu mtoto anapokuwa nyumbani kwao. Hapa kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuifanyia kazi changamoto ya tatu inayohusu dhamana na wajibu wa Jumuiya katika mchakato wa kurithisha elimu. Jambo linalotiliwa mkazo na Mama Kanisa ni ushirikiano unaojikita katika kanuni ya auni, kama sehemu ya Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Kardinali Parolin anasema, changamoto nyingine inayojitokeza katika mfumo wa elimu kwa sasa ni ujenzi wa dhana ya upinzani na uharibifu, kiasi hata cha kushindwa kuthamini utu na heshima ya binadamu. Huu ni uhuru usiokuwa na mipaka unaoshindwa kuthamini tofauti zinazojitokeza kati ya watu. Jamii haina budi kujikita katika mchakato wa elimu inayotafuta mafao ya wengi, haki na amani. Hii ni elimu inayopaswa kuzingatia kanuni maadili, umoja na udugu.

Askofu mkuu Francesco Follo, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO anakazia kwa namna ya pekee, umuhimu wa kuheshimu na kuthamini zawadi ya uhai katika mchakato wa elimu. Kuelimisha uwe ni mchakato wa kuwapatia vijana wa kizazi kipya ufahamu, ujuzi na maarifa yatakayowasaidia kujenga na kuimarisha dhamiri nyofu kwa kujenga utamaduni unaotambua utu na hehima ya binadamu. Elimu iwe ni chombo cha huduma kwa binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.