2015-06-10 08:38:00

Baada ya miaka 50, Wakristo Falme za Kiarabu wapata Kanisa la pili!


Katika maadhimisho ya Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu chemchemi ya faraja na huruma ya Mungu, sanjari na Siku kuu ya kuombea Utakatifu wa Mapadre, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anatarajiwa kutakabaruku Kanisa la Mtakatifu Paulo lililojenga hivi karibuni huko Abu Dhabi, kwenye Falme za Kiarabu. Hili ni Kanisa ambalo limejengwa katika eneo la viwanda ili kuwawezesha wafanyakazi wahamiaji kushiriki katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa.

Taarifa zinaonesha kwamba, Kanisa hili litafunguliwa rasmi hapo tarehe 11 Juni 2015 na Sheikh Nahyan Bin Mubarak Al Nahyan, Waziri wa vijana, tamaduni na maendeleo ya jamii Falme za Kiarabu. Askofu mkuu Petar Rajic, Balozi wa Vatican kwenye Falme za Kiarabu na viongozi mbali mbali wa Kanisa na Serikali wanatarajiwa kushiriki katika tukio hili la kihistoria, miaka hamsini baada ya Kanisa la kwanza kujengwa kwenye Falme za Kiarabu.

Kanisa la Mtakatifu Paolo lina uwezo wa kuwahudumia watu elfu tano kwa wakati mmoja. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya Wakristo millioni moja kwenye Falme za Kiarabu, lakini wengi wao ni wageni na wahamiaji wanaofanya kazi katika sekta mbali mbali za maisha nchini humo. Hali ya maisha na utume wa Kanisa mahalia ni nzuri na inatia moyo na inahamasisha ujenzi wa tunu msingi za maisha ya kifamilia. Falme za Kiarabu kwa sasa zinajielekeza zaidi katika ulimwengu wa utandawazi, ili kujenga mahusiano mema, yatakayosaidia kukuza na kudumisha amani na maridhiano kati ya watu, nyenzo msingi katika ukuaji wa kiuchumi na kijamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.