2015-06-09 16:02:00

Tambueni dhamana ya mshikamano na udugu, ili kulinda na kutunza mazingira


Vatican inashiriki kikamilifu katika Onesho la Chakula Kimataifa linaloendelea huko Milano, kaskazini mwa Italia, maarufu kama Expo Milano 2015 kwa kuwa na banda lake la maonesho. Lengo ni kuwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kugundua na kutambua dhamana ya mshikamano na udugu; ili kwa pamoja waweze kusimama kidete: kulinda na kuendeleza mazingira kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Kanuni hizi ni msingi ili kutoa matumaini kwa Familia ya mwanadamu.

Kardinali Gianfranco Ravasi, Rais wa Baraza la Kipapa la Utamaduni, Alhamisi, tarehe 11 Juni 2015 majira ya jioni anatarajiwa kuratibu majadiliano yanayoongozwa na kauli mbiu “Nyuso za Watu Duniani” na kuwashirikisha watu maarufu kama Guliano Amato na mwananzingira kutoka Ufaransa Bwana Nicolas Hulot, aliyeteuliwa na rais Hollande wa Ufaransa kuwa mwakilishi wake maalum kwenye mkutano wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika mjini Paris, Ufaransa mwezi Desemba 2015.

Utunzaji bora wa mazingira ni dhamana nyeti kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu wote, kama anavyobainisha Mtakatifu Francisko katika wimbo wake juu ya mazingira. Dunia ni mama mkarimu, mwenye utajiri mkubwa kama utatumiwa kwa ajili ya mafao ya wengi, kwa kuongozwa na kanuni auni, udugu na mshikamano, kwa hakika baa la njaa na umaskini vinaweza kupewa kisogo. Kimsingi, kuna uhusiano mkubwa kati ya ardhi na maisha ya binadamu; fursa na changamoto mbali mbali.

Katika historia ya maisha ya binadamu, kumekuwepo na matukio kadhaa yaliyosababisha majanga asilia na hivyo kuleta maafa makubwa katika maisha ya watu na mali zao. Lakini, hadi leo hii, baa la njaa na umaskini ni kati ya mambo yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Kuna watu ambao hawana uhakika wa usalama wa maisha yao kutokana na baa la njaa, lakini kwa upande mwingine kuna watu wanaokula na kusaza, kiasi cha kufanya kufuru!

Dunia itaendelea kuwa ni mama mwema na mkarimu anayetoa chakula na maji, lakini bado kashfa ya njaa na utapiamlo wa kutisha inawaelemea watu wengi duniani, kutokana na ubinafsi, ugavi mbaya wa chakula na utandawazi usioguswa na mahangaiko ya watu wengine.  Yote haya yatajadiliwa na kupembuliwa kwa kina na Kardinali Giafranco Ravasi pamoja na wageni wake huko Milano.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.