2015-06-09 15:12:00

Mshuhudieni Kristo kwa njia ya matendo yenu pasi na kumezwa na malimwengu!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumanne, tarehe 9 Juni 2015, amewataka waamini kukumbatia utambulisho wao wa Kikristo pamoja na kumwachia Roho Mtakatifu ili aweze kuwasindikiza katika hija ya maisha yao hapa duniani. Waamini waendelee kutoa nafasi kwa Roho Mtakatifu ili aweze kuyapyaisha maisha yao yanayojikita katika ushuhuda pasi na kumezwa na malimwengu.

Waamini wajitahidi kuwa waaminifu kwa Neno la Mungu walilolipokea katika maisha yao, ili Mwenyezi Mungu aweze kutukuzwa, kuheshimiwa na kuabudiwa. Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, ili kufikia hatua hii ya utambulisho wa Kikristo, Mwenyezi Mungu amefanya hija ndefu sana katika historia na maisha ya binadamu, kiasi hata cha kumtuma Mwanaye wa Pekee, Yesu Kristo, ili aweze kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Waamini wanatambua kwamba, ni wadhambi, lakini wana imani na matumaini ya huruma na upendo wa Mungu unaosamehe na kuokoa, changamoto kwa Wakristo kutekeleza dhamana hii katika maisha na utume wao kwa njia ya ushuhuda, hata kama wakati mwingine wanakumbana na giza katika safari hii ya maisha ya kiroho. Dhambi ni kikwazo kinachomwangusha mwamini katika safari yake ya maisha, lakini Mwenyezi Mungu anaweza kumnyanyua tena kwa nguvu mpya, kiasi cha kusonga mbele katika utambulisho wake, kama Mkristo, yaani Mfuasi amini wa Yesu Kristo.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, imani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambayo kwa njia ya Roho Mtakatifu waamini wanaimarishwa, tayari kuitolea ushuhuda, kwani tayari Mwenyezi Mungu amepiga chapa ya kudumu katika mioyo yao, chapa ambayo inawapatia utambulisho wa Kikristo. Huu ni mwaliko wa kuwa waaminifu katika utambulisho huu kwa kuunganika na Roho Mtakatifu anayetenda kazi ndani mwao.

Utambulisho wa Kikristo ni dhana nyeti na wala si jambo la kujisikia tu, bali imani inayomwilishwa katika ushuhuda wa maisha kama lugha na utambulisho wa Mkristo. Vishawishi na dhambi zipo na zitaendelea kuwepo, kumbe, waamini hawana budi kuhakikisha kwamba, wanakua imara na thabiti katika maisha yao ya kiimani kwa njia ya ushuhuda makini. Heri za Mlimani ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo yanayopaswa kumwilishwa kama kielelezo cha imani tendaji.

Baba Mtakatifu anaonya kwamba, ikiwa kama Wakristo watamezwa na malimwengu, watambue kwamba, wanapoteza utambulisho wao kama Wakristo na hivyo hii inakuwa ni kashfa katika maisha yao. Hata leo hii kuna wakanimungu; watu wanaotaka kuona mabadiliko kila kukicha na kusahau kwamba, wamepakwa mafuta na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo. Watu wanatafuta kuona miujiza na kwamba, Yesu Kristo ndiye Neno wa Mungu, kikomo cha ubishi wote.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, pale Wakristo wanapomezwa na malimwengu wanasumbuliwa na dhamiri tepetevu, isiyoweza kuchukua maamuzi  mazito katika maisha kwa kuchagua mema ili kuyakumbatia na mabaya kuyaachilia mbali. Ukristo wa kweli unajikita katika ushuhuda wa maisha unaoambata Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo.

Huu ndio utambaulisho wa Mkristo anayepaswa kufuata nyayo za Yesu Kristo aliyejinyenyekesha akazaliwa, akateswa na kufa Msalabani, ushuhuda wa upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu. Waamini wajitahidi kuomba neema ya kumshuhudia Kristo katika uhalisia wa maisha yao, kama chumvi ya ulimwengu na mwanga wa mataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.