2015-06-08 15:28:00

Waandishi wa habari wanapaswa kulindwa wanapotekeleza wajibu wao!


Askofu mkuu Bernardito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa wakati akichangia mada kuhusu umuhimu wa kuwalinda waandishi wa habari wanaotekeleza majukumu yao kwenye maeneo ya vita, ameonesha mshikamano wa upendo kwa familia ambazo zimeathirika kwa kuondokewa na wapendwa wao waliokuwa wanatekeleza kazi katika maeneo ya vita. Jamii ina haki ya kufahamu kile kinachoendelea katika uwanja wa mapambano na kusaidia mchakato wa kudumisha demokrasia, ili kuenzi Jumuiya ya binadamu.

Askofu mkuu Auza anasema kwamba, waandishi wa habari ni muhimu sana katika kutoa habari zinazohusiana na vita, maamuzi yanayotolewa pamoja na kubainisha mikakati inayoweza kutumika kwa ajili ya kukomesha vita. Kwa mwaka 2014 pekee, waandishi wa habari 69 walipoteza maisha na wengine 221 kufungwa gerezani. Na kwa mwaka 2015 hadi sasa kuna waandishi wa habari 25 waliokwisha uwawa na wengine 156 kufungwa gerezani, changamoto kwa pande zinazohusika kuhakikisha kwamba, zinawalinda waandishi wa habari ili waweze kutekeleza wajibu wao.

Kutokana na kupanuka kwa sayansi na maendeleo ya teknolojia ya habari, watu wengi wana hamu ya kupata habari kutoka katika maeneo ya vita, ili kujenga na kudumisha mshikamano wa kimataifa na waathirika wa vita kwa kuwapatia msaada wanaohitaji. Lakini wakati huo huo, watunga sera wanapata shida sana kupata habari za uhakika kutoka katika maeneo ya vita. Waandishi wa habari hawana budi kujikita katika kutangaza ukweli kwa ajili ya mafao ya wengi na kwamba, wahusika wa mauaji ya waandishi wa habari wafikishwe kwenye mkondo wa sheria, ili haki iweze kutendeka.

Askofu mkuu Auza anakazia kusema kwamba, waandishi wa habari hawana budi kulindwa wanapokuwa katika maeneo ya vita na kwamba, kuna haja ya kuangalia kama sera na mikakati ya kuwalinda waandishi wa habari kwa sasa inakwenda na wakati. Ni dhamana na wajibu wa Serikali kuwalinda waandishi wa habari na Jumuiya ya Kimataifa kwa upande wake isaidie kuwagharimia waandishi wa habari katika masuala ya fedha na uchumi. Waandishi wa habari wawe wa kwanza kujilinda wenyewe wanapokuwa vitani, kwa kujikita katika ukweli kwa kudumisha tunu msingi za maisha ya kiutu, kitamaduni na imani. Lengo msingi ni kuhakikisha kwamba, amani, utulivu na maridhiano vinapatikana na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa isimame kidete kuzuia vita, kinzani na migogoro.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.