2015-06-08 09:49:00

Rais Kirchner wa Argentina na ujumbe wake wakutana na Papa Francisko


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili jioni, tarehe 7 Juni 2015 amekutana na kuzungumza kwa faragha na Bi Cristina Fernàndes de Kirchner, Rais wa Jamhuri ya Argetina. Mazungumzo haya anasema Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican kwamba yamefanyika katika hali ya utulivu, pembeni kidogo mwa Ukumbi wa Paulo VI. Rais Kirchner ameonesha shukrani zake za dhati pamoja uwepo wa karibu wa Familia ya Mungu nchini Argetina kwa Baba Mtakatifu Francisko pamoja na kuomba baraka, neema na ustawi kwa ajili ya wananchi wake.

Baada ya mazungumzo haya, Baba Mtakatifu aliweza kusalimiana na msafara wa Rais Kirchner pamoja na wajumbe wa Argentina wanaoshiriki katika mkutano wa thelathini na tisa wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO unaoendelea mjini Roma. Pamoja na kukutana na viongozi wakuu wa Italia, Rais Kirchner anatembelea pia Onesho la Chakula kimataifa Expo Milano 2015.

Padre Lombardi anasema kwamba, Rais Cristina Fernàndes de Kirchner amemzawadia Baba Mtakatifu Francisko zawadi mbali mbali zenye umuhimu na kumbu kumbu ya pekee. Zawadi ya kwanza ni Picha ya Mwenyeheri Askofu mkuu Oscar Arnulfo Romero, iliyochorwa na msanii kutoka Argentina. Amempatia Kitabu kilichoandikwa na Bwana Alberto Methol-Ferrè pamoja na zawadi nyingine nyingi. Baba Mtakatifu Francisko kwa upande wake amempatia zawadi ya Picha ya Bikira Maria kutoka Russia, iliyochorwa kunako karne ya kumi na moja. Hii ni mara ya tano kwa Rais Cristina Fernàndes de Kirchner wa Argentina kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.