2015-06-08 10:57:00

Mshikamano, umoja na udugu miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali ni muhimu


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 7 Juni 2015 amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumwezesha kufanya hija ya kitume nchini Bosnia-Erzegovina, Jumamosi tarehe 6 Juni 2015 kama hujaji wa amani na matumaini mjini Sarayevo, unaopaswa kuitwa Yerusalemu ya Magharibi. Katika miaka ya hivi karibuni, mji huu umekuwa ni alama ya vita na maafa makubwa kwa binadamu.

Kwa sasa kuna mchakato wa upatanisho ambao umemsukuma kwenda kutembelea ili kuwatia shime wananchi wa Bosnia-Erzegovina kujielekeza katika njia ya maridhiano kati ya watu tofauti wanaoishi nchini humo. Hii ni safari yenye karaha na ugumu, lakini inawezekana. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru viongozi wa Serikali na wananchi wote wa Bosnia-Erzegovina kwa moyo wa ukarimu na mapokezi makubwa waliyomwonesha wakati alipowatembelea.

Kwa namna ya pekee, anaishukuru Jumuiya ya Wakatoliki, aliyewapelekea upendo wa Kanisa la kiulimwengu. Anawashukuru waamini wa dini mbali mbali kwa moyo wa mshikamano na udugu, hasa katika mchakato wa utekelezaji wa upatanisho wa maisha ya kiroho na kimaadili ndani ya jamii. Baba Mtakatifu anauombea baraka mji wa Sarayevo na nchi ya Bosnia-Erzegovina baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ili waendelee kushikamana kama ndugu wamoja

Baba Mtakatifu Francisko anakumbusha kwamba, Ijumaa ijayo, Kanisa linaadhimisha Siku kuu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, siku ambayo pia imetengwa kwa ajili ya kuombea utakatifu wa Mapadre. Moyo Mtakatifu wa Yesu ni kielelezo cha hali ya juu cha upendo na huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu anasema pia kwamba, tarehe 12 Juni 2015, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Kupambana Kazi za Suluba miongoni mwa watoto wadogo.Kuna umati mkubwa wa watoto sehemu mbali mbali za dunia ambao hawana uhuru wa kucheza wala kwenda shule na matokeo yake wanajikuta wakiishia mikononi mwa wadhulumati wanaowafanyisha kazi za suluba. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itaendelea kukazia na kudumisha haki msingi za watoto.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.