2015-06-08 09:09:00

Mapambano dhidi ya utakatishaji wa fedha haramu na ufadhili wa kigaidi


Mamlaka ya habari za kifedha mjini Vatican, Aif,  katika taarifa ya fedha kwa mwaka 2014 inasema kwamba,  mwelekeo wa sasa unaendelea kujikita katika umakini na ushirikiano; mambo ambayo yameimarishwa katika miaka ya hivi karibuni. Haya yamo kwenye taarifa ya Mamlaka ya habari za fedha mjini Vatican iliyotolewa hivi karibuni na Bwana Renè Brulhart, Rais wa Mamlaka pamoja na Bwana Tommaso di Ruzza, mkurugenzi mkuu wa mamlaka haya, hivi karibuni wakati walipokuwa wanazungumza na waandishi wa vyombo vya habari mjini Vatican.

Mamlka ya habari za kifedha ilianzishwa ili kupambana na wimbi la utakatishaji wa fedha haramu pamoja ufadhili wa vitendo vya kigaidi. Taarifa ya mwaka 2014 inaonesha kwamba, sheria na kanuni za fedha zimeendelea kuimarishwa katika taasisi mbali mbali zinazoendeshwa na Vatican. Kumekuwepo na ushirikiano mkubwa na vyombo vya ulinzi na usalama katika mapambano dhidi ya mchakato wa utakatishaji wa fedha haramu.

Bwana Renè Brulhart anasema kwamba, kwa sasa wamekamilisha mpango mzima unaopania kudhibiti vitendo vya kutakatisha fedha haram kwa kuwekeana makubaliano ya ushirikiano na nchi nyingine 13, kati ya nchi hizi ni: Italia, Ufaransa, Uingereza, Ujerumani, Marekani na Lussenburg. Ushirikiano wa kimataifa umeimarishwa zaidi baada ya kupata taarifa zilizokuwa zinahusiana na mzunguko wa fedha haramu kwa mwaka 2012. Kunako mwaka 2013 kulikuwa na taarifa 202 idadi ya taarifa hizi ilipungua na kufikia taarifa 147 ya mzunguko wa fedha haramu kunako mwaka 2014.

Haya ni mafanikio ya mchakato wa kudhibiti mzunguko wa fedha haramu kwa kujikita katika sheria na kanuni za masuala ya fedha. Taarifa inaonesha kwamba, kuna matukio saba ambayo tayari yamewasilishwa kwenye vyombo vya sheria mjini Vatican ili yaweze kufanyiwa uchunguzi wa kutosha na mamlaka husika. Idadi ya kesi zinazoshughulikiwa na Mamlaka ya habari za kifedha mjini Vatican pamoja na wadau kutoka nje ya Vatican zimeongezeka kutoka kesi 4 kwa mwaka 2012 hadi kufikia kesi 81 kwa mwaka 2013 na kwa mwaka 2014 kesi hizi zimeongezeka na kufikia 113.

Hizi ni juhudi zinazofanywa na Mamlaka hii kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama mjini Vatican anasema Bwana Di Ruzza. Madhumuni makubwa ni kudhibiti mchakato wa utakatishaji wa fedha haramu katika ngazi ya kimataifa. Idadi ye fedha iliyokuwa inapelekwa nchi za nje imeshuka kwa kiasi kikubwa na zile ambazo zilikuwa zinaingia imepungua pia. Mamlaka na vyombo vya ulinzi na usalama vimeendelea kuwa macho na makini kwa kuzingatia kanuni na sheria za masuala ya fedha.

Mamlaka hii pia imefanya ukaguzi  kwa muhula wa kwanza kwenye Benki ya Vatican, IOR ili kuangalia utekelezaji wa kanuni,  sheria na mbinu zilizowekwa ili kuzuia mchakato wa utakatishaji wa fedha haramu na ufadhili kwa vitendo vya kigaidi vinavyoweza kufanywa kwa kutumia Benki ya Vatican. Busara na hekima ni kati ya mambo muhimu yanayoendelea kutumiwa na Mamlaka ya habari ya fedha mjini Vatican.

Taarifa inaonesha kwamba, Vatican kwa sasa ina viwango vya kimataifa vinavyozingatia ukweli na uwazi; sheria na kanuni za fedha, kwa kutambua kwamba, fedha inapaswa kutumika kama kichocheo cha maendeleo na huduma kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa. Mamlaka itaendelea kufanya maboresho ya mchakato wa kudhibiti utakatishaji wa fedha haramu kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili katika ngazi ya kitaifa na kimataifa pamoja na kujikita katika sheria za fedha mjini Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.