2015-06-08 08:43:00

Katekesi makini na Uinjilishaji mpya ni sawa na uji kwa mgonjwa!


Waamini wanaendelea kuhamasishwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Unjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mashiko na mvuto, kielelezo cha imani inayomwilishwa katika matendo, Wakristo hawana budi kutoka kifua mbele tayari kuwatangazia watu wa mataifa Injili ya Furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa. Hapa waamini wajenge na kudumisha utamaduni wa watu kukutana kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko.

Katekesi makini na endelevu ni chombo muhimu sana katika mchakato wa Uinjilishaji mpya unaotambua upendo wa huruma ya Mungu kwa watu wake, wanaohamasishwa ili kweli waweze kuwa ni vyombo vya wokovu kwa ndugu na jirani zao. Katekesi anasema Baba Mtakatifu Francisko ni fursa makini inayomwezesha mwamini kukuza na kuimarisha imani kwa kutambua na kuonja huruma ya Mungu katika hija ya maisha yake.

Hapa familia na jumuiya za Kikristo zinapaswa kuwa ni maeneo ya kwanza kabisa ya kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni changamoto ya kimwilisha upendo na huruma ya Mungu katika uhalisia wa maisha. Ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko kwa siku za hivi karibuni ameshiriki kikamilifu katika mkutano wa Baraza la Sinodi za Maaskofu lililokuwa linapembua kwa kina na mapana kuhusu hati ya kutendea kazi ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya familia itakayoadhimishwa mwezi Oktoba hapa mjini Vatican.

Kardinali Odilo Pedro Scherer, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la San Paolo, Brazil anasema kwamba, hati ya kutendea kazi kwa sehemu kubwa imekamilika na itaweza kuchapishwa na kusambazwa wakati wowote kuanzia sasa. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa familia. Hati ya kutendea kazi, Instrumentum Laboris ni matunda ya mchango kutoka kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia na wadau wenye dhamana ya kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Injili ya Familia.

Kanisa kwa kuzingatia mafundisho tanzu, imani na Mapokeo yake, litaweza kupambanua sera na mikakati inayopaswa kufuatwa katika dhamana ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Familia duniani. Familia zenyewe zitambue kwa kina na mapana wito na utume wao katika Kanisa na ulimwengu mamboleo.

Kardinali Scherer anasema, Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji mpya linaendelea kuandaa muswada kuhusu: Katekesi na Uinjilishaji mpya, ili kuwasaidia waamini kuwa na nyenzo itakayowawezesha kutekeleza dhamana ya Uinjilishaji mpya  kwa urahisi zaidi sanjari na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.