2015-06-08 10:44:00

Ekaristi Takatifu ni muhtasari wa Fumbo la Msalaba na Sadaka endelevu ya Kristo


Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuhitimisha hija yake ya kitume nchini Bosnia-Erzegovina jumamosi jioni amerejea tena mjini Vatican ili kuendelea na utume wake kama kawaida. Jumapili, tarehe 7 Juni 2015 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana amekumbusha kwamba, Mama Kanisa sehemu mbali mbali za dunia ameadhimisha Sherehe ya Ekaristi Takatifu, maarufu kama “Corpus Domini”. Siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, wakati wa karamu ya mwisho, Yesu aliweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, yaani Mwili na Damu yake Azizi, kiwe ni chakula cha maisha ya uzima wa milele na uwepo wake endelevu kati ya waja wake.

Karamu ya mwisho ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha maisha na utume wa Yesu, muhtasari wa Fumbo la Msalaba na sadaka ya maisha yake kwa ajili ya ukombozi wa binadamu. Ekaristi Takatifu ni ishala ya uwepo endelevu wa Yesu unaopaswa kumwilishwa katika sadaka ya maisha inayowashirilisha waja wake. Waamini wanaposhiriki chakula hiki cha kimungu wanafanyika kuwa ni sehemu ya maisha ya Kristo, tayari kujenga mahusiano ya dhati kati yao, ili kweli maisha yao, yawezekugeuzwa kuwa ni sadaka kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Ekaristi Takatifu ni chemchemi ya upendo kwa maisha ya Kanisa, shule ya upendo na mshikamano. Waamini wanaoshiriki kikamilifu Fumbo la Ekaristi Takatifu wanapaswa kuguswa na mahangaiko ya jirani zao ambao wanateseka kutokana na baa la njaa. Hili ni tatizo na changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa, licha ya juhhudi zote zilizokwisha kupatikana. Hapa kuna haja ya kupembua na hatimaye, kubainisha mbinu mkakati na miradi mahususi ili kupambana na baa la njaa kutokana katika kiini chake.

Baba Mtakatifu anasema, Sherehe ya Mwili na Damu Azizi ya Yesu Kristo iwe ni fursa, dhamana na changamoto ya ujenzi wa jamii inayojikita katika moyo wa ukarimu, upendo na mshikamano wa dhati. Baba Mtakatifu anayaweka matumaini haya katika Moyo Safi wa Bikira Maria, Mama wa Ekaristi Takatifu. Apende kuamsha ndani ya waamini furaha ya kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, hususan siku za jumapili pamoja na kuwa na ushujaa wenye furaha ili kushuhudia upendo wa Kristo usiokuwa na mipaka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.