2015-06-08 14:50:00

Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha upendo, huruma na uwepo endelevu wa Kristo


Maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu yamekuwa ni fursa ya kuimarisha imani, matumaini na mapendo kwa Yesu wa Ekaristi ambaye aliwaambia wafuasi wake kwamba, atakuwa pamoja nao hadi utimilifu wa dahali. Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha upendo na huruma ya Yesu, ambaye anaendelea kufanya hija na wafuasi wake katika uhalisia wa maisha yao.

Hii inaonesha kwamba, kamwe Wakristo si pweke, kwani kwa njia ya Fumbo la Ekaristi Takatifu linalopaswa kusadikiwa, kuadhimishwa na kumwilishwa, Yesu anaendelea kufanya hija na waja wake. Ni safari ambayo imesheheni magumu na changamoto nyingi za maisha; lakini waamini wanahamasishwa kubaki wakiwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, kwa kutambua kwamba, Yesu mwenyewe atawapatia chakula cha mbingu, ili kuendelea na safari hadi kufikia lengo la maisha, yaani uzima wa milele.

Haya yamesemwa na Patriaki Fouad Twal wa Yerusalemu wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi takatifu, kama kielelezo cha ujumbe wa matumaini, wakati huu Wakristo wengi wanapokabiliwa na mateso, nyanyaso na mauaji. Ni watu wanaoendelea kutembea katika jangwa la maisha, kama ilivyokuwa kwa Waisraeli katika Agano la Kale.

Yesu Kristo, Mwanakondoo na Mkate wa uzima wa milele anawalisha na kuwategemeza wafuasi wake katika shida na magumu ya maisha, jambo la msingi ni wao kuwa na imani, matumaini na mapendo. Ibada hii ya Misa takatifu imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Kaburi Takatifu la Yesu mjini Yerusalemu. Hija ya Wakristo huko Mashariki ya Kati anasema Patriaki Twal inakabiliwa na changamoto na vizingiti vingi, lakini wakumbuke kwamba, wanaendelea kutegemezwa na sala za waamini na watu wenye mapenzi mema kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Ni matumaini ya Patriaki Twal kwamba, sala ya pamoja iliyowakutanisha viongozi wakuu kutoka Israeli na Palestina, itaweza kumwilishwa katika uhalisia wa maisha, tayari kujikita katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya Waisraeli na Wapalestina. Waamini wanaendelea kulishwa kwa chakula cha mbinguni, mkate wa malaika pamoja na kuimarishwa kwa njia ya Fumbo la Msalaba, wataweza kupata njia inayowaelekeza katika furaha, imani na matumaini.

Patriaki Twal amewakumbuka Wakristo sehemu mbali mbali za dunia wanaoendelea kuuwawa, kudhulumiwa na kunyanyasika kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha umoja na kifungo cha upendo kati ya wafuasi wa Kristo. Wakristo katika Ibada hii, wameombea amani, umoja, upendo na mshikamano kati ya watu, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu: kiroho na kimwili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.