2015-06-08 11:32:00

Baba Mtakatifu Francisko "achonga" na waandishi wa habari akiwa njiani!


Kanisa liko mbioni kutoa maamuzi kuhusu Medjugorje, dhamana na changamoto ya kuhamasisha amani na ulaji wa kutisha miongoni mwa vijana ni kati ya mada nyeti zilizogusiwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati akizungumza na waandishi wa habari, alipokuwa anarejea kutoka katika hija yake ya kitume nchini Bosnia-Erzegovina, Jumamosi, tarehe 6 Juni 2015. Baba Mtakatifu aliweza kusalimiana na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake na baadaye akajibu maswali machache waliyomuulizia.

Baba Mtakatifu Francisko anabainisha kwamba, kuhusu kesi ya Medjugorje, tayari kumefanyika upembuzi yakinifu na tume iliyoteuliwa na Papa mstaafu Benedikto XVI, chini ya usimamizi na uongozi wa Kardinali Camillo Ruini. Kumbe, Baraza la Kipapa la Mafundisho tanzu ya Kanisa linaendelea kutafakari taarifa iliyotolewa na Tume ya Kardinali Ruini, ili Kanisa liweze kutoa maamuzi ya kina kwa siku za usoni.

Baba Mtakatifu Francisko alipoulizwa kuhusu hija zake za kichungaji Barani Ulaya ambazo hadi sasa amezielekeza zaidi katika nchi zilizoko pembezoni mwa Ulaya kama vile Albania, Bosnia-Erzegovina anasema, kwamba, hizi ni dalili zinazoonesha utayari wake wa kuanza kutembelea nchi mbali mbali za Ulaya, lakini kwa kuanzia kwenye nchi ndogo ambazo katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, zimekumbana na vita, kinzani na majanga mbali mbali. Kumbe, lengo ni kuwatia ari na moyo wa kujikita katika mchakato wa ujenzi wa amani, maridhiano na mshikamano wa kitaifa.

Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, ni unafiki mkubwa kuzungumzia kuhusu amani, usalama na maridhiano kati ya watu, wakati huo huo kuna watu wanaoendelea kufanya biashara haramu ya silaha. Amani inajengwa katika majadiliano yanayojikita katika ukweli, haki, mafao ya wengi na maridhiano kati ya watu. Kamwe amani haiwezi kuhubiriwa kwa njia ya biashara ya silaha.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, vijana wanapaswa kuwa makini na kuwajibika vyema na matumizi ya vyombo vya mawasiliano ya kijamii kama vile: televisheni, computer na simu za viganjani, vinginevyo wanaweza kujikuta kwamba, wanakuwa ni watumwa wa mambo haya. Vyombo hivi vya mawasiliano ya jamii, badala ya kuunganisha familia, vinaanza kuonesha dalili za kuleta utengano na mpasuko wa kifamilia.

Hata familia zinapokuwa mezani, kila mtu anahangaika na simu yake, kiasi kwamba, hakuna tena mawasiliano ya kina kati ya wanafamilia. Mitandao ya kijamii ni ukweli usiopingika, lakini watu wanapaswa kuwa na busara na matumizi ya kiasi ya vyombo hivi kwa ajili ya mafao ya tunu msingi za maisha ya kifamilia na kiutu. Kuna baadhi ya mitandao ya kijamii imekuwa ni shimo la takataka kwa kuonesha picha chafu, ili kuwavuta vijana; baadhi ya vituo vya televisheni vinawatumbukiza watu katika nadharia ya anasa na starehe pamoja na mawazo mepesi mepesi: mambo ambayo yanachangia kuporomosha tunu msingi za maisha ya kimaadili, kiutu na kiroho.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Waraka wake wa kichungaji kuhusu utunzaji bora wa mazingira utazinduliwa rasmi hapo tarehe 18 Juni 2015. Hapa anapenda pia kupembua kuhusu uchafuzi wa mazingira katika ekolojia ya mwanadamu. Busara inapaswa kutumika ili kudhibiti matumizi ya mabaya ya vyombo vya mawasiliano ya jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.