2015-06-07 08:32:00

Yakumbukeni mateso na madhulumu si kwa kulipiza kisasi, bali kujenga amani


Ushuhuda wa maisha ya wakleri na watawa wakati wa vita nchini Bosnia-Erzegovina uliotolewa mbele ya Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini humo, Jumamosi jioni tarehe 6 Juni 2015 umevuta hisia za wengi, kiasi hata cha kumfanya Baba Mtakatifu Francisko, kukabidhi hotuba aliyokuwa amewaandalia wakleri na watawa, ili iwasaidie kwa tafakari yao hapo baadaye, lakini akaanza kuwashirikisha yale ambayo yamemgusa. Huu ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko ambao hauna haja ya kuongeza wala kupunguza chochote.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, hii ni kumbu kumbu hai ya wananchi wa Bosnia-Erzegovina walioyakita maisha yao katika imani kwa Kristo na Kanisa lake. Wananchi hawa wanayo haki ya kukumbuka historia iliyopita, si kwa kutaka kulipiza kisasi, bali kujielekeza zaidi katika mchakato wa ujenzi wa amani na maridhiano kati ya watu. Ni mwaliko wa kuwaangalia, ili kupenda na kuthamini zawadi ya maisha inayomwilishwa katika wito na huduma kwa Familia ya Mungu.

Mashuhuda wa imani wanapaswa kukumbukwa na kuheshimiwa, kwani wao wamekuwa ni chemchemi ya imani ambayo imeendelee kububujika kwa njia ya ushuhuda wa maisha, lakini zaidi, wanapaswa kumkumbuka Yesu Kristo, aliyejisadaka kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Mashuhuda wa imani hata katika nyakati hizi wanaendelea kufuata nyayo za Yesu Kristo. Kumbukumbu ya mateso na mahangaiko ya Wakristo iwe ni chachu ya kuchuchumilia amani, msamaha na upatanisho.

Wakleri na watawa watambue kwamba, wamewekwa wakfu kuwa ni vyombo vya msamaha na huruma ya Mungu kwa waja wake. Si rahisi kusamehe, lakini ndani ya Kanisa kuna mashuhuda wa imani wanaodhihirisha kwamba, kusamehe ni jambo linalowezekana kumwilishwa katika uhalisia wa maisha. Kuna watu wameteseka sana katika kambi za mateso, lakini walipopata bahati ya kutoka huko, wakavikwa fadhila ya msamaha, hiki ni kielelezo cha maisha yanayofumbatwa katika Fumbo la Msalaba wa Yesu, utukufu na maisha ya wahudumu wa amani na matumaini.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, hata leo hii katika ulimwengu unaosheheni mauaji, chuki na kinzani za kidini, lakini kuna watu wenye imani thabiti katika upendo wa Mungu, kiasi kwamba, wako tayari hata kama ni waamini wa dini nyingine, kuonesha upendo na huruma kwa Wakristo wanaoteseka na kunyanyasika. Huu ni mwaliko wa kutafuta mafao ya wengi badala ya kujikita katika ubinafsi, kwani wote ni watoto wa Mungu, wameumbwa kwa sura na mfano wake.

Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza wakleri na watawa ambao wako karibu na mashuhuda wa imani, matumaini na mapendo. Kuna familia nyingi ambazo zimepoteza wapendwa wao katika vita, kinzani na vurugu nchini Bosnia-Erzegovina, sasa ni wakati wa kuchuchumilia tunu msingi za maisha ya kifamilia, ili kweli familia ziweze kuwa ni shule ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kidugu. Familia bora anasema Baba Mtakatifu ni kitalu cha miito mitakatifu ndani ya Kanisa. Wananchi wa Bosnia-Erzegovina wametikiswa sana na historia ya ukatili, lakini umefika wakati wa kuwa na mwelekeo mpya katika maisha, kwa kujikita katika upole, udugu na msamaha, huku wakiendelea kubeba kwa imani na matumaini, Msalaba wa Yesu katika maisha yao. Kanisa linawataka watoto wake kuwa kweli ni mashuhuda wa Msalaba wa Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.