2015-06-07 09:29:00

Wajengeeni vijana mazingira ya kufahamiana, kupendana na kuheshimiana!


Baba Mtakatifu Francisko, amehitimisha hija yake ya kitume nchini Bosnia-Erzegovina, Jumamosi jioni tarehe 6 Juni 2015 kwa kukutana na kuzungumza na vijana kutoka Bosnia-Erzegovina pamoja na nchi jirani. Tukio hili limefanyika kwenye Kituo cha Vijana Jimbo kuu la Sarayevo. Ameshiriki sala na kusikiliza shuhuda za vijana katika hija ya maisha yao kwa kutambua kwamba, fainali ya ujana wanaisubiri uzeeni.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa vijana wa kizazi kipya amepembua huduma msingi zinazotolewa na Mama Kanisa katika utume kwa vijana nchini humo na kukaza kwamba, Serikali pamoja na taasisi mbali mbali hazina budi kuhakikisha kwamba, zinatengeneza sera na mikakati makini itakayowajengea vijana uwezo katika masuala elimu, utamaduni, taaluma na uchumi, ili kudhibiti wimbi kubwa la nguvu kazi kukimbia nchini Bosnia-Erzegovina ili kutafuta malisho ya kijani kibichi nje ya nchi yao.

Kanisa Katoliki kwa njia ya mchakato wa Uinjilishaji mpya, kwa kutumia shule, taasisi na vyuo vikuu vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa  pamoja na mikakati mbali mbali ya shughuli za kichugaji miongoni mwa vijana, linapenda kusaidia majiundo makini kwa maisha ya wananchi wa Bosnia-Erzegovina katika masuala ya kimaadili na kiraia, ili kuwajengea uwezo vijana wa kizazi kipya waweze kuwa ni wadau na wachangiaji wakuu katika masuala ya kijamii.

Kabla ya yote, Baba Mtakatifu Francisko, anawataka vijana wa kizazi kipya kupambana kikamilifu na changamoto zinazoendelea kumwandama mwanadamu, kwa kuwa na mwono sahihi wa mtu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; kumong’onyoka kwa tunu na kanuni msingi za kimaadili, kiasi kwamba, mwanadamu amepoteza maana ya maisha. Kuna haja ya kutengeneza fursa za ajira ili vijana waweze kuwa na uhakika wa usalama na maisha yao kwa siku za usoni.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kutoka kifua mbele ili kushuhudia Ukristo wao kwa kutambua dhamana na changamoto zinazowakabili kwa sasa na kwa siku za usoni. Umakini huu anasema Baba Mtakatifu unawawezesha vijana kusimama kidete katika maisha yao bila kuanguka katika kishawishi cha kukimbia au kukwepa majukumu; kwa kukumbatia ubinafsi; au kwa kujikuta wakiwa ni “mateja” wa matumizi haramu ya dawa za kulevya au utamaduni unaowajengea watu chuki na uhasama.

Imani ya kweli inapata kielelezo chake kwa njia ya mshikamano wa dhati na Yesu Kristo, kwa kushiriki katika utume unaotaka kuwajengea watu matumaini, kwa kuangalia ukweli wa maisha na kujiandaa kikamilifu kwa siku za usoni katika mazingira yanayothamini utu na heshima ya binadamu na ukweli. Mambo haya anasema Baba Mtakatifu ni msingi wa wa ujenzi wa jamii inayojikita katika ukarimu pamoja na kuheshimiana katika tofauti zinazojitokeza tayari kushiriki na kudumisha ujenzi wa utamaduni wa upendo. Watu wote wanaitwa kuwa ni watoto wateule wa Mungu na ndugu zake Kristo. Hapa Baba Mtakatifu anapongeza jitihada zote zinazofanywa katika majadiliano ya kidini na kiekumene kwa kuwaunganisha vijana kutoka katika dini mbali mbali ili kufahamiana na kushirikiana na kidugu, tayari kujielekeza katika maridhiano, amani na utulivu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.