2015-06-07 10:38:00

Vijana tumieni vyema vyombo vya mawasiliano ili kulinda uhuru na utu wenu!


Baba Mtakatifu Francisko wakati akihitimisha hija yake ya kichungaji nchini Bosnia-Erzegovina, Jumamosi jioni, tarehe 6 Juni 2015, alipata nafasi ya kujibu maswali matatu yaliyoulizwa na vijana. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu amegusia kuhusu dhamana na wajibu wa vyombo vya mawasiliano ya jamii, katika mchakato wa kurithisha tunu msingi za maisha kiroho, kiutu na kijamii, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya mtu mzima na kamwe visiwe ni kwa ajili ya kumdhalilisha mwanadamu. Tunu hizi ziwasaidie vijana kujiandaa kikamilifu katika kukabiliana na changamoto za maisha.

Baba Mtakatifu anawaalika vijana kuwajibika barabara katika matumizi ya vyombo vya mawasiliano ya kijamii kwa kuhakikisha kwamba, wanachagua na kuangalia programu zenye kuwajenga na kuwaimarisha katika fadhila mbali mbali, wasikubali kuangalia takataka zote zinazosambazwa kwenye vyombo vya habari. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, wao ni wazee waliokulia katika kipindi cha vitabu, lakini hata wakati huo, walikuwa na uwezo wa kuchagua vitabu vya kusoma.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kuwa na matumizi sahihi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii kama vile computer na simu na wala wasigeuzwe kuwa ni watumwa wa vyombo hivi vinavyoweza kuwanyima uhuru wa kweli na utu wao kama binadamu. Vyombo vya mawasiliano ya jamii viwasaidie vijana kupata ujuzi, maarifa na weledi wa maisha, tayari kukua, kukomaa na kuwajibika katika safari ya maisha.

Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, daima vijana wamekuwa ni chemchemi ya furaha na matumaini katika maisha yake; ni matunda ya mapambazuko mapya katika maisha ya wananchi wa Bosnia-Erzegovina, mwaliko wa kusonga mbele pasi na kukumbatia tena utamaduni wa kifo, bali washikamane katika urafiki na udugu; wakionesha uzalendo na umoja wa kitaifa unaovuka mipaka ya kidini na kikabila; ili kujenga na kudumisha amani, maridhiano na umoja.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kamwe amani haitaweza kupatikana ikiwa kama bado kuna watu wanaoshabikia biashara haramu ya silaha kwa ajili ya mafao yao binafsi. Huu ni unafiki wa kuzungumzia amani, lakini hao hao wako mstari wa mbele kuuza silaha. Vijana wanapaswa kuwa ni wajenzi wa madaraja ya watu kukutana, kwa kujikita katika uaminifu, umoja na udugu.

Vijana wajengewe uwezo wa kuwa kweli ni vyombo vya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa. Hii ndiyo dhamana ambayo Baba Mtakatifu Francisko amependa kuwaachia vijana kutoka Bosnia-Erzegovina na nchi jirani waliokusanyika ili kumsikiliza na kubadilishana naye matumaini, furaha na mahangaiko yao ya ndani. Amani iwe ni zawadi kwa wananchi wote wa Bosnia-Erzegovina, ili wote waweze kuwa ni wamoja, kwa kumwabudu Mungu mmoja asili ya wema wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.