2015-06-07 08:58:00

Majadiliano ya kidini yajikite katika mafao ya wengi, kanuni maadili na uhuru


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Bosnia-Erzegovina, Jumamosi jioni tarehe 6 Juni 2015 amezindua Kituo cha Wanafunzi Kimataifa kilichowekwa chini ya ulinzi na usimamizi wa Mtakatifu Yohane Paulo II, mbele ya umati mkubwa wa vijana kutoka sehemu mbali mbali za Bosnia-Erzegovina. Hiki ni kituo ambacho kinatumika kama sehemu ya ujenzi wa utamaduni wa majadiliano ya kidini na kiekumene, kwa kuwakutanisha vijana kutoka katika dini na madhehebu mbali mbali ya Kikristo.

Katika kituo hiki, Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza na wawakilishi wa dini na madhehebu mbali mbali ya Kikristo nchini Bosnia-Erzegovina. Mkutano huu anasema Baba Mtakatifu Francisko ni kiu ya kutaka kujenga na kudumisha udugu na amani, kwa njia ya ushuhuda unaojikita katika urafiki.

Tofauti za kiimani na kidini ni rasilimali kubwa katika mchakato wa maendeleo katika medani mbali mbali za maisha ya binadamu baada ya kutikiswa na vita iliyopelekea umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia. Baraza la Majadiliano ya kidini lililoundwa kunako mwaka 1997 ni matokeo ya vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini humo, kama jibu sahihi katika mchakato wa upatanisho baada ya vita, Majadiliano ya kidini ni nyenzo muhimu sana katika ujenzi wa amani.

Baba Mtakatifu Francisko anabainisha kwamba, majadiliano ya kidini  licha ya kujikita katika masuala ya kiimani, yanagusa kwa namna ya pekee uhalisia wa maisha ya mwanadamu; katika furaha na shida, ili kufanya maamuzi ya pamoja kwa ajili ya mafao na ustawi wa wengi. Majadiliano yanawawezesha waamini wa dini mbali mbali kufahamiana, ili kwa pamoja waweze kusimama kidete, kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya kimaadili, uhuru wa kuabudu pamoja na kudumisha amani.

Majadiliano ya kidini ni shule ya ubinadamu; kikolezo cha umoja; mambo msingi yanayoiwezesha jamii kuwa na mardhiano pamoja na kuheshimiana. Kumbe, hii ni changamoto ya jamii nzima na wala si jukumu la watu wachache ndani ya jamii. Vijana wapewe kipaumbele cha kwanza. Viongozi wa kidini wanapaswa kuwa ni wajenzi na vyombo vya amani nchini Bosnia-Erzegovina. Kanisa Katoliki kwa upande wake, litaendeleza mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, kuna mambo mengi ambayo yanapaswa kutekelezwa ili amani ya kweli iweze kupatikana tena. Sarayevo utaendelea kuwa ni kielelezo cha vita na majanga katika maisha ya mwanadamu; lakini kwa upande mwingine unaonesha juhudi za wananchi wa Bosnia-Erzegovina katika ujenzi wa umoja na mshikamano katika tofauti, ili kwa pamoja waweze kujenga na kudumisha amani na udugu kati ya watu.

Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amesali sala ya kiekumene kwa kuomba huruma na msaada wa Mungu kwa ajili ya wananchi wa Bosnia-Erzegovina ili waweze kuishi kwa amani na utulivu; wakionjeshana upendo, ili kujenga haki ya kijamii, waoneshe moyo wa kusameheana kwa kujikita katika majadiliano, ili kweli amani ya kweli iweze kupatikana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.