2015-06-06 15:29:00

Simameni kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu, uhuru na amani!


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wa video aliowaandikia wananchi wa Bosnia-Erzegovina kuhusu hija yake ya kitume anasema, anapenda kuwaimarisha ndugu zake Wakatoliki katika imani, kuendelea kuhamasisha majadiliano ya kiekumene na kidini ili kujenga misingi ya amani na maridhiano. Amani iwe kwenu ndiyo kauli ambayo imeongoza hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini humo na kwamba, anapenda kuwa kweli ni mjumbe wa amani na huruma ya Mungu kwa waja wake.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa viongozi wa serikali, kisiasa, kidiplomasia na kidini nchini Bosnia-Erzegovina amekumbusha kwamba, mji wa Sarayevo uliathirika vibaya kutokana na vita iliyopelekea umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia, lakini mji huu leo hii ni kielelezo cha majadiliano, maridhiano na utulivu. Ni mji ambao kwa miaka mingi umekaliwa na waamini wa dini na madhehebu mbali mbali ya Kikristo. Hawa ni watu kutoka katika makabila, mapokeo na tamaduni mbali mbali, kielelezo cha utajiri mkubwa kwa wananchi katika mchakato wa ujenzi wa mahusiano mema.

Sarayevo ni mji ambao umesheheni nyumba za Ibada kwa waamini wa dini ya Kiislam, Kikristo na Kiyahudi, hapa ni kama mji wa Yerusalemu Barani Ulaya. Hii ni njia panda ya tamaduni, mataifa na dini mbali mbali, dhamana ambayo kwa namna ya pekee kabisa inahitaji ujenzi wa madaraja mapya sanjari na kufanya maboresho ya madaraja yaliyokuwepo, ili kuimarisha usalama na mawasiliano ya kijamii. Watu, familia na jumuiya mbali mbali ziwezeshwe kurithisha tunu msingi za maisha ya kitamaduni pamoja na kuwa tayari kupokea mema yanayotoka kwa wengine. Kwa njia hii, madonda ya chuki na vita yanaweza kugangwa na hatimaye, kuponywa.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, hija hii inafanyika, ikiwa imegota miaka 18 baada ya Papa Yohane Paulo II kutembelea Bosnia-Erzegovina, kunako mwaka 1997, miaka miwili baadaye, Mkataba wa Amani wa Dayton, ukatiwa sahihi. Tangu wakati huo, kumekuwepo na maendeleo makubwa katika mchakato wa ujenzi wa maelewano na maridhiano kati ya watu. Dhamana hii nyeti inahitaji ushirikiano wa dhati kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa, hususan Jumuiya ya Ulaya, ili kweli nchi ya Bosnia-Erzegovina iweze kuwa ni sehemu ya Umoja wa Ulaya, kwa kushirikisha matumaini na mahangaiko ya wananchi wake, tayari kujenga misingi ya amani na utulivu.

Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, amani kati ya makabila makuu ya Bosnia-Erzegovina, mahusiano mema, ushirikiano kati ya waamini wa dini mbali mbali ni muhimu sana katika kuchuchumilia mafao ya wengi; sanjari na kuendelea kusafisha dhamiri na kuponya madonda yaliyopita, ili kujenga matumaini mapya. Huu ni mwaliko wa kuondokana na sera zinazopania kuwatenga watu kwa misingi mbali mbali na badala yake, wananchi wajikite katika utambuzi wa misingi thabiti ya maisha ya mwanadamu kwa: kushirikiana, kujadiliana, kusameheana na kukua kwa pamoja badala ya kuendekeza chuki na visasi visivyo na tija wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya wananchi wa Bosnia-Erzegovina.

Baba Mtakatifu anawakumbusha viongozi wa kisiasa kwamba, dhamana na wajibu wao msingi ni kuhakikisha kuwa wanasimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu; lakini zaidi uhuru wa kidini, ili kujenga jamii inayosimikwa katika misingi ya haki na amani. Ili kufanikisha azma hii, kuna haja ya kudumisha usawa miongoni mwa wananchi wote kadiri ya sheria na utekelezaji wake; ili wananchi wote waweze kujisikia kwamba, wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa maisha ya hadhara, kwa kupata haki zao msingi zinazowawezesha kutoa mchango wao kwa ajili ya mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha hotuba yake kwa viongozi wa Serikali, siasa, kidiplomasia na kidini kwa kukazia mchango wa Kanisa katika Katoliki katika ujenzi wa jamii: kiroho na kimwili na kwamba, Vatican kwa upande wake, itaendeleza mchakato wa ujenzi wa amani na utamaduni wa kusikilizana, katika hali ya amani na utulivu vigezo muhimu sana katika mchakato wa maendeleo endelevu na dumifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.