2015-06-06 16:44:00

Sarayevo ni mji uloteseka, sasa ni kielelezo cha majadiliano na amani!


Baba Mtakatifu Francisko wakati akiwa njiani kuelekea Bosnia-Erzegovina amewatumia salam za matashi mema Marais wa Italia na Croatia. Anasema anakwenda Bosnia-Erzegovina ili kuhamaisha mchakato wa majadiliano kati ya tamaduni na dini mbali mbali ili kujenga umoja na mshikamano kati ya watu. Anapenda kuimarisha imani ya ndugu zake katika Kristo.

Hivi ndivyo Baba Mtakatifu alivyomwandikia ujumbe, Rais Sergio Mattarella wa Italia, wakati akiwa njiani kuelekea Bosnia-Erzegovina ambako amepata mapokezi ya kukata na shoka, kiasi cha kuwaacha watu wakiwa wameshika tama kwa mshangao mkubwa! Baba Mtakatifu anasema Italia na Jumuiya ya Ulaya katika ujumla wake, inaingalia hija hii ya kitume kwa jicho la matumaini, kwani anakwenda nchini humo kama mjumbe wa amani na upatanisho, ili kuganga na kuponya madonda ya chuki, kinzani na vita vilivyopelekea maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Baba Mtakatifu pia amemwandikia ujumbe wa matashi mema Rais Kolinda Gbara-Kitarovic wakati alipokuwa anapita kwenye anga la Croatia. Amewabariki wananchi wa Croatia, ili Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo awawezeshe kutembea katika njia ya amani, haki na mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu akiwa njiani kuelekea Bosnia-Erzegovina amepata nafasi kidogo ya kupiga mchapo na waandishi wa habari 65 kutoka katika nchi 10 wanaofanya kazi zao katika lugha tisa, ili kuhakikisha kwamba, ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko unawafikia watu wengi zaidi katika kukoleza mchakato wa ujenzi wa madaraja ya watu kukutana, kufahamiana, kuheshimiana na kusaidiana kama ndugu.

Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee, analishukuru na kulipongeza jopo la waandishi wa habari ambalo lina kazi kubwa kuhakikisha kwamba, watu wanapashwa habari li kufahamu kile kinachoendelea. Sarayevo anasema Baba Mtakatifu ni mji unaokaliwa na dini kuu tatu: Waislam, Wakristo na Wayahudi, ni kama Yerusalemu ndogo Barani Ulaya. Sarayevo ni mji wenye tamaduni, mapokeo na makabila mbali mbali. Ni mji ambao umeonja mateso makubwa, lakini kwa sasa uko katika njia ya amani. Baba Mtakatifu anasema, anafanya hija hii kama hujaji wa amani, majadiliano na mshikamano kati ya watu. Anawashukuru waandishi wa habari kwa moyo wao wa ushirikiano.

Na padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.