2015-06-06 15:43:00

Iweni vyombo na mafundi wa ujenzi wa amani katika uhalisia wa maisha!


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye uwanja wa michezo wa Kosevo, wakati wa hija yake ya kitume nchini Bosnia-Erzegovina, Jumamosi, tarehe 6 Juni 2015 amekazia kuhusu utajiri wa Liturujia ya Neno la Mungu iliyokuwa inakazia kwa namna ya pekee haki na amani na kwamba utimilifu wa haki ya kweli unajikita katika upendo kwa Mungu na jirani; muhtasari wa mafundisho makuu ya Yesu, anayekaza kusema: heri wapatanishi maana hao wataitwa wana wa Mungu. Lakini hali na mazingira yaliyopo kwa sasa inaonekana kana kwamba, dunia iko katika mapambano ya vita kuu ya tatu ya dunia.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, Mtakatifu Paulo katika Waraka wale kwa Wakolosai anaonesha  mikakati inayoweza kuwasaidia waamini kuwa kweli ni vyombo na wajenzi wa amani inayotekelezwa kwa vitendo, kwani hii ni kazi ya kiufundi inayofumbatwa katika moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, kwa kuchukuliana na kusameheana; mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo nanyi mnapaswa kusameheana.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, amani ni mradi ambao Mwenyezi Mungu ameufanya kwa ajili ya binadamu, historia na kwa ajili ya kazi nzima ya uumbaji. Lakini kwa bahati mbaya, zawadi hii ya Mungu imeendelea kukumbana na kinzani pamoja na vikwazo vinavyoibuliwa na binadamu mwenyewe pamoja na Shetani. Leo hii, sehemu mbali mbali za dunia kuna mtutu  wa bunduki unaendelea kurindima kama kwamba, hii ni vita kuu ya tatu ya dunia, athari zinazooneshwa na vyombo vya upashanaji habari.

Kuna baadhi ya watu wanaoendelea kufaidika kiuchumi na kisiasa kutokana na vita inayoendelea sehemu mbali mbali za dunia. Hawa ni wafanyabiashara wanaotaka kuuza silaha. Vita daima imekuwa ni chanzo kikuu cha majanga ya mwanadamu, lakini waathirika wakubwa ni watoto, wanawake na wazee wanaolazimika kupata hifadhi kwenye kambi za wakimbizi; kwenye maeneo ya watu wasiokuwa na makazi maalum. Vita inaharibu miundo mbinu kiasi cha kukwamisha maendeleo. Vita ni chanzo kinachopelekea watu wengi kupoteza maisha yao.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Yesu anawaambia wafuasi wake kuwa ni vyombo na wajenzi wa amani inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku. Hii inatokana na ukweli kwamba, kuna watu wengi wenye uwezo wa kuhubiri amani, lakini wakati mwingine mahubiri yao yanaficha unafiki uliomo mioyoni mwao. Ujenzi wa amani ni mchakato endelevu unaojikita katika ari, uvumilivu na uzoefu. Unahitaji udugu, majadiliano na huruma na kwamba, hatua kwa hatua, amani inakuwa ni utekelezaji wa haki.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha mahubiri yake kwenye Uwanja wa michezo wa Kosevo kwa kuwaambia waamini kwamba, haki inapatikana kwa kuimwilisha katika matendo ya upendo kwa Mungu na jirani kama anavyofundisha Yesu mwenyewe. Baada ya Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Papa Francisko na msafara wake ameungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Bosnia-Erzegovina kwa chakula cha mchana, kilichokuwa kimeandaliwa kwenye Ubalozi wa Vatican nchini humo. Hii imekuwa ni fursa pia kwa Maaskofu kuweza kubadilishana mawazo, mang’amuzi na vipaumbele vyao katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.