2015-06-05 15:45:00

Moyo Mtakatifu wa Yesu uliotobolewa ni chemchemi ya faraja, amani na wokovu


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 5 Juni 2015 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa Shirika la Mapadre wa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Amewapongeza Mapadre wote wanaotekeleza dhamana yao katika mazingira magumu na kuwataka kusonga mbele huku wakijikita katika uaminifu unaofumbatwa katika ukarimu. Mkutano mkuu ni nafasi kwa Jumuiya kutafakari na kumwilisha dhana ya upatanisho, ili kuweza kuwashirikisha wengine maisha na Injili, kwa kuonesha huruma ndani ya jumuiya pamoja na kuambatana na maskini.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka Mapadre hawa kukita maisha na utume wao katika Heri za Mlimani kwa kuwa ni watawa wenye huruma, wanaoboresha muungano wao na Mwenyezi Mungu kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu sanjari na maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, ili hija ya maisha yao iwasaidie kukua na kukomaa katika huruma, kwa kuonja upendo wa Mungu ili kufahamiana zaidi na wale wanaoishi nao.

Mchakato wa upyaisho wa maisha na utume wao, uwawezeshe kuwa kweli ni chemchemi hai ya watu kujengana na kutakatifuzana katika jina la Yesu, ambaye Moyo wake uliotobolewa ni chemchemi ya faraja, amani na wokovu kwa watu wote. Mapadre hawa wanakumbushwa kwamba, maisha ya kitawa ni hija ya pamoja ya waamini wanaojisikia kupendwa na wao wanajitahidi kuhakikisha kwamba, wanampenda Mwenyezi Mungu.

Watawa wajitahidi kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao ya Kijumuiya, kwa kuwa na huruma kwa ndugu zao pamoja na kufuata ushuhuda wa maisha ya mwanzilishi wao wa Shirika, Mtume wa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Huruma ni muhtasari wa Injili na sura ya Kristo aliyowaonesha wale wote waliobahatika kukutana naye, kwa kuponywa magonjwa, kusamehewa dhambi na kuwaonjesha upendo, ambao ulifikia kilele cha hali ya juu kabisa pale juu Msalabani.

Baba Mtakatifu anasema, upendo huu wanapaswa kuonjeshwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa njia ya ushuhuda wa pendo lililomiminwa ndani mwao kwa njia ya Roho Mtakatifu. Mtindo wa maisha yenye huruma utawasaidia kuwa ni vyombo makini vya Uinjilishaji kwa watu wa nyakati hizi, hata kama itawabidi kutoa sadaka, lakini hili ni jambo la lazima katika kuponya magonjwa ya nyakati hizi.

Baba Mtakatifu anawakumbusha Mapadre wa Moyo Mtakatifu wa Yesu kwamba, historia ya Shirika lao imejengeka kwenye msingi wa sadaka na ukarimu wa ndugu zao waliojifunga kibwebwe ili kuwa wahudumu wa Injili, kwa kushikamana na viongozi mahalia, wakawa moyo mmoja na roho moja katika ufukara. Wamissionari hawa waendelee kuwa ni mfano na kielelezo cha maisha, ari na hamasa ya kimissionari katika medani mbali mbali za utume wao. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, mkutano mkuu utawasaidia kuendelea kuwa waaminifu kwa karama ya mwanzilishi wa Shirika lao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.