2015-06-05 08:14:00

Kanisa katika kukabiliana na changamoto za maisha na utume wa wanawake!


Gazeti la L’Osservatore Romano linalomilikiwa na Vatican, hivi karibuni limeendesha semina ya kimataifa kuhusu dhamana na nafasi ya wanawake ndani ya Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake, semina ambayo imekamilishwa kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, katika maadhimisho ya Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Pamoja na mambo mengine, wajumbe wamepembua kwa kina na mapana tunu msingi ambazo zinaweza kusaidia kuimarisha maisha ya ndoa na familia; umuhimu wa wanawake na malezi kwa watoto wanaoasiliwa.

Sr. Clotilde Bikafuluka kutoka DRC ameshirikisha ushuhuda wa huduma inayotolewa kwa wanawake wanaokumbana na nyanyaso na dhuluma za kijinsia kutokana na vita inayoendelea huko DRC. Hizi ni ni kati ya changamoto za kutisha ambazo wanawake wanaotoka katika maeneo ya vita wanakabiliana nazo kila siku ya maisha, kiasi cha kuwakatisha tamaa na matumaini kwa siku za usono. Kuna wanawake na wasichana wanaoendelea kupoteza maisha yao kutoka na ukatili na unyama wanaofanyiwa na askari. Wanawake na wasichana hawa mara nyingi wanapata msaada na huduma kutoka katika vituo vinatoendeshwa na kusimamiwa na Makanisa.

Sr. Yudith Pereira Rico ambaye kwa muda wa miaka 17 anatekeleza utume wake nchini Sudan ya Kusini, anasema, waliamua kuanzisha mradi kwa ajili ya huduma kwa wanawake na wasichana ili kusikiliza kilio cha dhuluma na nyanyaso dhidi ya wanawake na wasichana waliokuwa wanateseka kutokana na mfumo dume, nyanyaso na dhuluma ambazo wakati mwingine zinafanyika katika kuta za kifamilia. Wasichana wengi wanajikuta wakilazimika kuingia kwenye ndoa za shuruti pasi na ridhaa yao wenyewe, matokeo yake ni mimba za utotoni na ongezeko kubwa la maambukizi ya magonjwa ya zinaa na Ukimwi.

Wanawake wasiojua kusoma wala kuandika nchini Sudan ya Kusini wanafikia walau asilimia 80% ya idadi ya wananchi wote wa Sudan ya Kusini, hali ambayo inatisha na kuhuzunisha. Ikumbukwe kwamba, elimu ni mkombozi wa wanyonge. Pamoja na changamoto zote hizi, bado wanawake wameendelea kuwa ni vyombo vya ujenzi wa haki, amani na maridhiano kati ya wananchi wa Sudan ya Kusini ambao bado wanaendelea kuangamia kutokana na vita inayosababishwa na uchu wa mali na madaraka.

Wajumbe mbali mbali wanakiri kwamba, katika maisha na utume wa Yesu, alileta mabadiliko makubwa katika maisha na utume wa wanawake wa nyakati zake, kiasi cha kuwapatia majukumu mazito, kinyume kabisa cha tamaduni na fikira za watu wa nyakati zake. Kanisa linatambua na kuthamini umama wa wanawake kama Madhabahu matakatifu ya maisha ya binadamu, changamoto ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Uhai ambayo kwa sasa inakabiliwa na utamaduni wa kifo unaojikita katika sera na mikakati ya utoaji mimba pamoja na kifo laini.

Wajumbe wanakiri kwamba, leo hii kuna watu ambao wanaogopa kupokea dhamana na majukumu ya maisha ya ndoa na familia na matokeo yake ni kuzuka kwa uchumba sugu pamoja na kuporomoka kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zinazojikita katika upendo thabiti kati ya bwana na bibi. Ulaya ni kati ya Mabara ambayo yana idadi kubwa ya mimba zinazotolewa, ikifuatiwa na India na China.

Vita, umaskini, njaa na magonjwa ni kati ya matatizo makubwa yanayowaandama wnawake wanaoishi katika nchi changa zaidi duniani; mambo ambayo yanaendeleza pia unyanyasaji na dhuluma za kijinsia zinazotendwa katika kuta za kifamilia. Lakini tatizo hili linaendelea kupanuka na kuongezeka hata katika nchi tajiri zaidi duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.