2015-06-05 07:51:00

Ekaristi Takatifu ni nguvu ya wanyonge na wadhambi; alama ya msamaha na upendo


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu, Alhamisi, tarehe 4 Juni 2014 ameongoza bahari ya watu katika Ibada ya Misa takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Yohane wa Laterano. Maadhimisho ya Misa takatifu, Ibada ya Kuabudu Ekaristi pamoja na maandamano makubwa ya Ekaristi Takatifu yaliyopambwa kwa tafakari ya Neno la Mungu, nyimbo za Ekaristi kuelekea kwenye Kanisa kuu la Bikira Mkuu, lililoko mjini Roma. Mara baada ya maandamano kuwasili, Baba Mtakatifu aliwapatia baraka ya Ekaristi Takatifu.

Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu Francisko anasema, wakati wa Karamu ya mwisho, Yesu aliwapatia wafuasi wake Mwili na Damu yake azizi kama chakula cha njiani, katika historia ya ujenzi wa ufalme wa Mungu. Hii ndiyo sadaka ya upendo aliyoionesha kwa njia ya sadaka ya Fumbo la Msalaba. Mkate wa uzima umewafikia hata waamini wa nyakati hii na kwamba, Kanisa linaendelea kushangaa ukweli huu. Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha uwepo endelevu wa Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu.

Waamini wanaposhiriki Mkate huu wa uzima, wanafanyika kuwa ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo na kwamba, Ekaristi takatifu ni kifungo chau pendo na huruma ya Mungu. Waamini wanahamasishwa kushikamana na Yesu kwa kuwa wasikivu wa Neno lake, kwa kujenga na kudumisha umoja na udugu pamoja na kujitahidi kuwa wanyenyekevu. Ni changamoto ya kumshuhudia kwa njia ya matendo ya upendo kwa kuwajengea wengine matumaini.

Ekaristi Takatifu ni kifungo chau pendo na utimilifu wa Agano Jipya; alama wazi ya upendo wa Yesu Kristo aliyejinyenyekesha hata akajisadaka ili aweze kuungana na wafuasi wake pasi na kugawanyika. Yesu anaendelea kuonesha uwepo wake kwa njia ya Ekaristi Takatifu anayetaka nguvu ya upendo wake ivunjilie mbali aina zote za mipasuko ili kuungana na wafuasi wake ambao wakati mwingine wanaelemewa na ubinadamu wao, kiasi hata cha kuwa hatarini kupoteza zawadi ya imani.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, Ekaristi Takatifu inawakirimia waamini utu na heshima ya kuitwa Wakristo, changamoto ya kuondokana na miungu inayoweza kuwazingua katika maisha na kujikuta wakimezwa na ubinafsi, mashindano yasiyokuwa na mashiko wala mguso, kiburi na hali ya kujiamini kupita kiasi kana kwamba, hawahitaji msaada wa mtu awaye yote; haya ni mambo ambayo yanawafanya Wakristo kurudia tena upagani.

Yesu alimwaga Damu yake azizi ili kuwasafisha waja wake na dhambi zao, ili kuwaunganisha tena, mwaliko wa kukimbilia chemchemi ya maisha mapya, ili wasimezwe na malimwengu, tayari kupokea neema iliyowaletea mabadiliko na kuwarejeshea utu wao. Kwa njia ya unyenyekevu, Wakristo wanaweza kuwaonjesha jirani zao upendo wa Yesu Kristo Mkombozi.

Waamini wawe ni macho ya Yesu yanayomtafuta Zakayo mtoza ushuru na Magdalena; wawe ni mkono wa Yesu unaotoa huduma kwa wagonjwa wa kiroho na kimwili; wawe ni Moyo wa Yesu unaowapenda wale wote wanaotamani kuonja tena huruma, upatanisho na wema wa Mungu. Ekaristi Takatifu inakamilisha agano na kuwatakatifuza waamini, ili hatimaye, waweze kuungana na Mwenyezi Mungu. Fumbo la Ekaristi Takatifu ni nguvu ya wanyonge na wadhambi; ni kielelezo cha msamaha na chakula cha njiani kinachowawezesha waamini kutembea na kusonga mbele.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Sherehe ya Ekaristi Takatifu inawawezesha waamini kuadhimisha Fumbo hili kuu kwa kulitukuza na kuimba nyimbo za shangwe, huku wakiandamana na Yesu wa Ekaristi mitaani mwao. Hii ndiyo ile hija iliyofanywa na Mwenyezi Mungu kwa kutembea na waja wake katika jangwa la umaskini wa mioyo yao, ili kutoka katika kongwa la utumwa na hatimaye, kushibishwa na upendo unaobubujika kutoka katika Mwili na Damu yake Azizi.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini wanapofanya maandamano ya Ekaristi Takatifu, kuwakumbuka na kuwaombea waamini ambao hawana uhuru wa kuabudu, ili kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Waamini waungane na watu hawa katika sala, nyimbo na Ibada ya kuabudu. Wawakumbuke na kuwaombea wale wote walioshuhudia uaminifu wao kwa Kristo, ili damu yao iliyomwagika, ikiungana na Damu azizi ya Yesu iwe ni chemchemi ya amani na upatanisho kwa ulimwengu wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.