2015-06-05 08:36:00

Adhabu ya kifo imepitwa na wakati ni kinyume cha haki msingi za binadamu!


Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani limepokea kwa furaha kubwa uamuzi uliofanywa na Gavana wa Jimbo la Nebraska wa kufuta adhabu ya kifo jimboni mwake, kama kielelezo cha kukumbatia mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa maisha. Pongezi hizi zimetolewa na Askofu Thimas G. Wenski, Mwenyekiti wa Tume ya haki, amani na maendeleo ya Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani.

Anasema,haiwezekani kufundisha kwamba, mauaji ni tendo baya kwa kuendelea kuua. Kanisa linapenda kuungana na watu wote ambao kwa miaka mingi wamesimama  kidete kupinga adhabu ya kifo pamoja na kutambua masikitiko ya ndugu na jamaa ambao wamepoteza maisha yao kutokana na mauaji. Haki haiwezi kupatikana  kwa kuwanyima wengine haki ya kuishi.

Kanisa linapenda kuwahimiza na kuwafundisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema, umuhimu wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Maisha ya binadamu ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, yanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa, tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu.

Adhabu ya kifo ilirejeshwa tena nchini Marekani na Mahakama kuu kunako mwaka 1976. Tangu wakati huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani pamoja na watu wenye mapenzi mema, wanaokumbatia na kuthamini Injili ya Uhai, wameendelea kupinga adhabu ya kifo, inayotekelezwa hadi wakati huu katika majimbo 31 nchini Marekani.

Kanisa linatambua na kufundisha utakatifu na ukuu wa maisha ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Adhabu ya kifo, haijafanikiwa kupunguza mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, kumbe kuna haja ya kutafuta adhabu mbadala inayoheshimu utu na maisha ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.