2015-06-04 08:43:00

Injili ya Familia Barani Afrika: Uzuri, fursa, matatizo na changamoto zake!


Furaha na changamoto za maisha ya ndoa na familia; wito, tasaufi na utume wa familia, dhamana na utume wa Maaskofu katika mchakato wa utangazaji wa Injili ya Familia ni kati ya mambo msingi ambayo yametiliwa mkazo na wajumbe wa Semina ya ndoa na famlia iliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM pamoja na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, CCEE, huko Maputo, Msumbiji. Semina hii imeongozwa na kauli mbiu “Furaha ya familia”.  Hii ni semina ya nne kuendeshwa kwa pamoja tangu Mashirikisho haya yalipoanza ushirikiano wake kunako mwaka 2004.

Wajumbe wa semina hii wametumia muda mwingi kutafakari juu ya wito na utume wa familia ndani ya Kanisa na Ulimwengu mamboleo, kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia itakayoadhimishwa hapa mjini Vatican kuanzia tarehe 4 hadi 25 Oktoba 2015. Katika kupembua furaha ya familia, wajumbe wamewakumbuka ndugu na jamaa zao, walivyoshiriki kikamilifu katika mchakato wa kurithisha tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu; msingi ambao unaendelea kuwaimarisha kama Maaskofu, licha ya magumu na changamoto zilizojitokeza.

Familia ni mahali ambapo watu wanashirikishana tone la upendo katika maisha ya ndoa kati ya bwana na bibi na kwamba, watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu, wanaopendwa na kurithishwa tunu msingi za maisha ya kiroho. Hapa ni mahali pa kushirikiana kwa dhati, kusamehe na kusameheana kwa kutambua kwamba, kukosa na kukoseana ni sehemu ya ubinadamu, changamoto ya kutoa msamaha na upatanisho, tayari kusonga mbele kwa imani na matumaini.

Maaskofu kwa kutambua kwamba, wanayo dhamana ya kuwa kweli ni wachungaji wema, wanasema wanaguswa sana na mahangaiko ya familia mbali mbali zinazoteseka kutokana na ukata wa maisha; umaskini, magonjwa pamoja na kukosekana kwa huduma makini katika sekta ya afya. Wanatambua kwamba, kuna familia ambazo zina watoto walioathirika kutokana na matumizi haramu ya dawa za kulevya; wazazi na ndugu wanaofanya kazi mbali na familia; familia zinazoteseka kutokana na vita na kinzani.

Maaskofu wanasema bado kuna familia ambazo zinalazimika kukimbilia uhamishoni kutokana na sababu mbali mbali, bila ya kuwasahau watu wanaotumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu. Wanasikitishwa kuona makundi makubwa ya watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira hatarishi; watoto wanaotumbukizwa katika uhalifu wa magenge na utumwa mamboleo. Inasikitisha kuona watu wanakata tamaa kiasi hata cha kukumbatia utamaduni wa kifo kwa njia ya sera za utoaji mimba.

Maaskofu wanakiri kwamba, licha ya matatizo na changamoto zote hizi, bado Roho Mtakatifu anaendelea kutenza kazi ndani ya familia, kwani kuna familia nyingi ambazo zinaendelea kutangaza na kushuhudia Injili ya Familia inayojikita katika Injili ya Uhai, kwa kupokea na kutunza zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kuna sera na mikakati mingi inayopania kuimarisha misingi ya ndoa na familia. Huu ni mwanzo wa matendo makuu ya Mungu kwa ajili ya Familia ya binadamu..

Bara la Afrika linaheshimiwa sana kutokana na ukweli kwamba, linathamini zawadi ya maisha, mwaliko kwa familia kuendelea kushikamana katika sala, maadhimisho ya Sakramenti mbali mbali za Kanisa, hususan Sakramenti ya Ekaristi Takatifu inayoziwezesha familia kupata chakula cha kiroho, amani na utulivu; tayari kukumbatia mchakato wa utakatifu wa maisha. Wazazi wanakumbushwa kwamba, wanayo dhamana nyeti ya kuhakikisha kwamba, wanawarithisha watoto wao tunu msingi za maisha ya kiutu; wanajenga mawasiliano katika: utu, ukweli na uwazi, ili kukabiliana na changamoto mamboleo.

Ni wajibu wa Serikali na watunga sera kuhakikisha kwamba, wanazisaidia familia kutekeleza dhamana na wito wao kikamilifu, kwa ajili ya mafao ya jamii. Watoto na vijana wasaidiwe kupata mang’amuzi bora zaidi ili kutambua kilicho cha kweli, cha haki na fadhila ili kuepuka mabaya. Familia za Kikristo zijenge na kuimarisha wito wake wa kimissionari, kwa kujikita katika ukarimu, majadiliano na utamadunisho; ili kuwafunda watoto ili waweze kuwa kweli ni matumaini ya jamii kwa siku za usoni.

Maaskofu wanasema kwamba, dhamana yao kubwa ni kuwapelekea Yesu, ambaye anaendelea kuwaonesha uso wa upendo na huruma, ili kuziwezesha familia kukua na kukomaa katika upendo na imani na kwamba, uwepo wa Bikira Maria iwe ni faraja kwa wapweke, wagonjwa na wote waliotengwa. Familia, kamwe zisielemewe na ubinafsi na dhambi. Wazazi wawasaidie vijana wao kujiandaa barabara kupokea na kumwilisha Injili ya Familia katika uhalisia wa maisha yao. Maaskofu wanasema, watajitahidi kuuendeleza utume huu pamoja na kuwasaidia wanandoa wazee na wale waliotengana kuonja tena huruma na upendo wa Kristo unaobubujika kutoka kwa Kanisa lake.

Maaskofu wanahitimisha tamko lao kwa kuwataka wanafamilia kufurahi daima katika Bwana, ili upole na wema wao uweze kujulikana na wote; wawe ni watu wa sala; kwa kuomba na kushuruku mbele ya Mungu, daima wawe ni watu wa amani, kwa kujikita katika mambo ya kweli, yenye staha, yaliyo ya haki, safi, yenye kupendeza na kuwa na sifa njema. Watende yale wanayofundishwa na Kanisa na kwa njia hii, Mungu wa amani atakuwa pamoja nao daima.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.