2015-06-04 15:10:00

Amani ni zawadi kutoka kwa Mungu inayomwajibisha mwanadamu!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Kituo cha Televisheni cha Vatican, CTV anabainisha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anafanya hija ya kitume nchini Bosnia-Erzegovina ili kuihamasisha familia ya Mungu nchini humo kujikita katika kutafuta na kudumisha mafao ya wengi, kwa njia ya urafiki unaojengeka katika udugu, majadiliano na amani. Hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini humo inaongozwa na kauli mbiu, “amani iwe kwenu”. Kanisa linatambua kwamba, amani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomwajibisha mwanadamu.

Bosnia-Erzegovina  ni nchi ambayo  kwa miaka mingi ilijikuta ikiogelea katika vita ya wenyewe kwa wenyewe, iliyosababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Vita iliwagawa wananchi kwa misingi ya kikabila na kidini, wakashindwa kushikamana kama ndugu wamoja. Ndiyo maana kauli mbiu ya hija hii ya kitume ni “amani kwenu”, salam ambayo Yesu Kristo mfufuka aliwapatia wafuasi wake, Jioni ya Siku ya kwanza ya juma wanafunzi walipokuwa wamejifungia ndani kwa woga wa Wayahudi.

Baba Mtakatifu Francisko anafanya hija hii kama hujaji wa majadiliano na amani, ili kuweza kuganga na kuponya madonda ya kinzani na vita, iliyosababisha watu wengi kupoteza maisha yao na wengine kulazimika kuyakimbia makazi kwa kuhofia usalama wa maisha yao. Madhara ya vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini humo yanajionesha kwa namna ya pekee miongoni mwa Wakristo waliokuwa zaidi ya laki nane, leo hii wamebaki waamini laki nne. Kuna baadhi ya Parokia zimebaki na familia chache kabisa zinazohudumiwa na wazee.

Kardinali Parolin anasema kwamba, vijana wengi wanaishi uhamishoni, kutokana na ukosefu wa fursa za ajira na kazi, kumbe wanajikuta wakilazimika kutafuta maisha bora zaidi nje ya nchi yao. Idadi ya watoto wanaozaliwa ni ndogo sana, jambo hili pia linachangia kwa Jumuiya ya Wakatoliki kuendelea kudumaa zaidi. Hii ni changamoto kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuchuchumilia Injili ya Familia inayojikita katika Injili ya Uhai.

Bosnia-Erzegovina ni nchi ambayo inakaliwa na makabila makuu matatu: Wabosnia, Waserbia na Wakroashia. Kutokana na muundo huu wa kijamii, hapa kuna haja ya kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kina ili kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa na kwamba, tofauti zao ni sehemu ya utajiri wa wananchi wote wa Bosnia-Erzegovina, kumbe wanapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa kuimarisha amani na maridhiano kati yao.

Bosnia-Erzegovina inaweza kuwa ni kielelezo cha mshikamano wa dhati kwa mataifa ambayo yanaendelea kuchechemea katika mchakato wa ujenzi wa mshikamano wa kitaifa kutokana na vita, kinzani za kijamii na tofauti zinazojitokeza kwa misingi ya kikabila na kidini. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anatumani kwamba, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini humo itasaidia kwa kiasi kikubwa mchakato wa wananchi kushikamana kwa ajili ya kutafuta mafao ya wengi pamoja na kuendelea kuboresha hali ya maisha ya wananchi. Huu ni mwaliko kwa wananchi wote wa Bosnia-Erzegovina kuchuchumilia misingi ya haki, amani, upatanisho, ustawi na maendeleo ya wote: kiroho na kimwili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.