2015-06-03 15:31:00

Waamini waombea mchakato wa Mw. J.K. Nyerere kutangazwa Mwenyeheri!


Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 3 Juni anafanya kumbukumbu ya Mashahidi 22 wa Uganda walichomwa moto kunako mwaka 1886 kwa amri ya Kabaka Mwanga. Wakatangazwa kuwa wenyeheri na Papa Benedikto wa kumi na tano kunako mwaka 1920. Baba Mtakatifu Paulo VI akawatangaza kuwa wenyeheri tarehe 18 Oktoba 1964. Ujasiri wao wa imani ni mbegu iliyopandwa katika mioyo ya waamini wengi ndani na nje ya Uganda.

Leo hii kuna umati mkubwa wa waamini unaofanya hija ya maisha ya kiroho kwenye Madhabahu ya Mashahidi wa Uganda, huko Namgongo, ili kuomba imani, matumaini na mapendo katika hija ya maisha yao ya Kikristo. Katika kipindi cha miaka tisa sasa, maadhimisho ya Siku kuu ya Mashahidi wa Uganda, imekuwa pia ni fursa kwa ajili ya kuombea mafanikio katika mchakato wa kumtangaza Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kutoka Tanzania kuwa Mwenyeheri na hatimaye Mtakatifu kadiri ya mapenzi ya Mungu.

Kabla ya kilele cha maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Mashahidi wa Uganda, kwenye Kanisa dogo la Namugongo, kumefanyika Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Padre Lawrence Kenyi, kutoka Chuo kikuu cha Kyambogo. Katika mahubiri yake amesema kwamba, Mwalimu Nyerere alikuwa ni mwaminifu kwa Mungu na Kanisa, akawa ni mfano na kielelezo cha imani na uchaji uliokuwa unamwilishwa katika uhalisia wa maisha yake.

Mwalimu Nyerere alisimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu, akapinga uonevu na unyanyasaji wa aina mbali mbali. Ni kiongozi aliyejenga umoja na mshikamano wa kitaifa; akawajali wanyonge na kuwainua maskini; akawafariji wote waliotafuta hifadhi nchini Tanzania kutoka sehemu mbali mbali za Bara la Afrika.

Mahujaji kutoka Tanzania wametakiwa kumuenzi Baba wa taifa kwa njia ya ushuhuda unaomwilishwa katika matendo. Ibada hii ya Misa Takatifu imehudhuriwa na Mama Maria Nyerere pamoja na familia yake. Ni matumaini ya Familia ya Mungu Afrika Mashariki kwamba, iko siku, Mtumishi wa Mungu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere atatangazwa na Kanisa kuwa niĀ  Mwenyeheri na hatimaye, Mtakatifu.

Kwa upande wake, Ruhakana Rugunda, Waziri mkuu wa Uganda aliyemwakilisha Rais Yower Kaguta Museven katika Ibada hii, amemtaja Mwalimu Nyerere kuwa ni kiongozi na mfano wa kuigwa Barani Afrika. Anastahili kutangazwa kuwa Mwenyeheri na hatimaye Mtakatifu, kwani alichangia kwa namna ya pekee kulinda, kutetea utu na heshima ya watu wengi Kusini mwa Bara la Afrika.

Mwalimu Nyerere anakumbukwa kuwa ni kati ya viongozi maarufu kutoka Barani Afrika. Wengine ni: Kwame Nkurumah, Mzee Nelson Mandela, Samora Machel, Mzeee Jomo Kenyatta, Rais Gamel Abdel Nasser na wengine wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, kwa msaada wa magazeti ya Uganda.








All the contents on this site are copyrighted ©.