2015-06-03 15:00:00

Umaskini unavyotikisa msingi wa maisha na tunu bora za kifamilia!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano, tarehe 2 Juni 2015 amegusia umaskini na athari zake katika familia, hasa zile familia zinazoishi pembezoni mwa miji mikuu, bila kusahau familia zilizoko vijijini. Wakati mwingine familia zinajikuta zimetumbukia katika umaskini mkubwa kutokana na vita, mama ya umaskini wote  duniani; inayosababisha pia majanga makubwa katika maisha ya mwanadamu. Lakini pamoja na changamoto na magumu ya maisha, kuna baadhi ya familia ambazo zinajikabidhi kwa ulinzi na tunza kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa kuishi kadiri ya uwezo na mazingira yao.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, ni muujiza na jambo la kushangaza kuona kwamba, hata katika umaskini, bado familia zinaendelea kuundwa na kudumishwa. Jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, wanasiasa na watunga sera wanatoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao ya watu binafsi dhidi ya ustawi na maendeleo ya familia. Wakristo wanahamasishwa kusimama kidete kulinda, kutetea, kutangaza na kushuhudia Injili ya Familia; kwa kuonesha mshikamano wa dhati na familia maskini.

Kanisa ni Mama na Mwalimu na kamwe hawezi kufumbia macho mateso na mahangaiko ya watoto wake. Hapa kila mwamini anapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake katika mapambano dhidi ya umaskini kwa kuvunjilia mbali kuta za utengano, ili hatimaye, baa la umaskini liweze kupewa kisogo. Kanisa maskini, litaweza kuzaa matunda yanayokusudiwa kwa watoto wake wengi wanaohitaji msaada.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kusali kwa ajili ya kuombea wongofu wa ndani, ili familia za Kikristo sehemu mbali mbali za dunia ziweze kuwa ni vyombo vya kuwasaidia ndugu zao wanaoteseka katika umaskini. Anaziweka familia zote katika huruma na upendo wa Mungu. Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, Mwezi Juni, Kanisa linafanya Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Sherehe ya Ekaristi takatifu iwe ni chachu kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa Ekaristi kwa ajili ya jirani zao, lakini zaidi kwa ajili ya familia maskini zaidi.

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu ametuma salam na matashi mema kwa vijana kutoka Poland wanaokutanika huko Lednica, ili kuonesha mshikamano wao na Yesu Kristo pamoja na kuendelea kumwilisha karama na mapaji waliyopokea kutoka kwa Roho Mtakatifu. Waamini wanachangamotishwa kumfungulia Roho Mtakatifu malango ya mioyo yao, ili awajaze kwa mapaji yake.

Waamini wamwombe Roho Mtakatifu ili aweze kuwasindikiza wawapo kazini, masomoni, katika sala na wanapofanya maamuzi, kwa ajili ya mafao ya wengi. Roho Mtakatifu anawajalia waamini maisha ya kweli, anaponya upweke unaowaandama waja wake, anawasindikiza na kuwaongoza, pale wanapompatia nafasi. Waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kukua  na kukomaa katika maisha ili kupata utimilifu wa upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Waamini wakumbatie utakatifu wa maisha kwa kujishikamanisha na nguvu ya Roho Mtakatifu anayewajalia upendo mkomavu na unaowajibika na upendo wenye nguvu kuliko hata kifo.

Baba Mtakatifu amewapongeza vijana wanaokimbiza Mwenge wa Amani, ili tukio hili liweze kuwa kweli ni kikolezo cha kujikita katika mchakato wa amani na mshikamano na wote wanaohitaji msaada zaidi. Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa mahujaji na waamini kutoka China na ametumia fursa hii kuwahakikishia uwepo wake wa karibu wakati huu mgumu wanapoendelea kulia na kuomboleza kutokana na ajali ya Boti iliyozama kwenye Mto Yangtze hivi karibuni na kusababisha watu wengi kupoteza maisha na wengine bado hawajulikani mahali walipo.

Boti hiyo ilikuwa imebeba abiria 458 kati yao ni abiria 18 tu waliokolewa wakiwa wazima, wengine wengi wanahofiwa kwamba, wamekufa maji. Chanzo cha ajali hii ni kutokana na hali mbaya ya hewa. Baba Mtakatifu anawaombea wale wote waliofikwa na msiba huu mzito.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.