2015-06-03 07:42:00

Mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa amani kati ya watu wa mataifa!


Dini mbali mbali duniani zina dhama na wajibu wa kujenga, kudumisha na kuendeleza utamaduni wa amani na maridhiano kati ya watu kama kichocheo kikuu cha maendeleo na ustawi wa watu. Vita imekuwa ni chanzo kikuu cha majanga yanayoendelea kuwakumba watu wengi duniani, kiasi cha kuwatumbukiza hata katika umaskini wa hali na kipato, licha ya kunyanyasa na kudhulumu utu na heshima ya binadamu. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanabainisha kwamba, amani haina budi kuchukuliwa katika mapana yake na wala si ukosefu wa vita.

Vita kuu ya kwanza na ya pili ya dunia ni matukio ambayo Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na tano aliyaita kwamba ni matukio yasiyokuwa na maana, kumbe, Jumuiya ya Kimataifa kwa kushirikiana na wadau mbali mbali haina budi kuhakikisha kwamba, chokochoko na vita vinadhibitiwa mapema kabla ya kusababisha majanga kwa watu na mali zao. Wahenga wanasema, vita haina macho, inawakumbuka waliomo na wasiokuwemo na madhara yake ni makubwa hata kwa wale wasiohusika.

Huu ni mchango ambao umetolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican alipokuwa anachangia mada kwenye kongamano la kimataifa kuhusu mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa amani na mchango wa dini katika kudumisha amani duniani. Anasema, Kanisa lina dhana ya kuendelea kuhamasisha mchakato wa ujenzi wa umoja, udugu, amani na maridhiano kati ya watu. Jumuiya ya Kimataifa inafanya kumbu kumbu ya vita kuu ya pili ya dunia, ili kuwasaidia vijana wa kizazi kipya waweze kuchuchumilia amani na kamwe wasitumbukie na hatimaye kuonja madhara ya vita.

Baba Mtakatifu Francisko akizungumzia kuhusu vita anakazia kusema kwamba, kuna haja ya kujenga utamaduni wa amani katika haki, ukweli na upendo. Vita kamwe si nyenzo ya kurejesha haki iliyopokwa, na matokeo yake, vita inakuwa ni mwendelezo wa ukosefu wa haki, kumbe, kuna haja ya kujikita katika mchakato unaopania kuzuia na kusitisha vita inayoweza kujitokeza katika mifumo mbali mbali. Leo hii nchi mbali mbali duniani zinakabiliwa na vita, kumbe, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujielekeza zaidi katika majadiliano katika ukweli, uwazi na kwa ajili ya mafao ya wengi. Jumuiya ya Kimataifa ijifunze madhara ya vita yanayoendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Umoja wa Mataifa una dhamana kubwa ya kuhakikisha kwamba, amani na usalama vinatawala duniani. Lakini ukweli wa mambo unaonesha kwamba, hata Umoja wa Mataifa umeshindwa kutekeleza dhamana hii ambayo ilikuwa ni sababu ya kuundwa kwake. Diplomasia ya kimataifa inaonekana kushindwa na hatimaye, Umoja wa Mataifa unatekeleza dhamana hii katika misingi ya ushirikiano na mshikamano. Amani ya kweli ni utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho, unaozingatia utu wa binadamu, mafao ya wengi na uhuru wa kweli. Imani inamwezesha mwanadamu kutekeleza majukumu yake na kwamba, amani ni dhana inayowezekana, ikiwa kama kila mtu atatekeleza dhamana na wajibu wake.

Askofu mkuu Gallagher anasema kwamba, inasikitisha kuona kuwa katika baadhi ya maeneo, dini zinakuwa ni chanzo cha vita, vurugu na kinzani za kijamii. Lakini wachunguzi wa mambo wanabainisha kwamba, vita na migogoro hii, nyuma yake kuna watu wanaofaidikika kiuchumi na kisiasa na dini zinatumiwa kama chombo cha kutekelezea matakwa yao binafsi, ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko anawataka viongozi wa kidini kukemea na kulaani dini kuwa ni chanzo cha vita na kinzani za kijamii. Mauaji kwa misingi ya kidini ni kufuru dhidi ya Mwenyezi Mungu ambaye ni asili ya wema na utakatifu wa maisha.

Viongozi wa kidini wanao wajibu na dhamana ya kujenga utamaduni wa amani, haki na maridhiano kati ya watu. Jumuiya ya Kimataifa inaweza kusaidia kufundisha vijana wa kizazi kipya umuhimu wa kukuza na kudumisha amani, ili baadaye wao wenyewe waweze kuwa ni vyombo na wajenzi wa amani. Kuna haja pia ya kudhibiti biashara haramu ya silaha duniani ambayo inaendelea kunuka harufu ya damu ya watu wasiokuwa na hatia. Dini ziwasaidie watu kujenga dhamiri nyofu kwa kutambua mema wanayopaswa kuyakumbatia na maovu ya kuyakataa kwa kutumia kanuni maadili na utu wema.

Askofu mkuu Gallagher anabainisha kwamba, Chama cha kitume cha Pax Christi, kilichoanzishwa nchini Ufaransa mara baada ya Vita kuu ya Pili ya Dunia ni kielelezo tosha cha mchango wa Kanisa katika ujenzi wa utamaduni wa amani. Kanisa linatambua kwamba, amani ya kweli inafumbatwa katika: toba, msamaha, upatanisho na sala; mambo ambayo yanapaswa kupata chimbuko lake katika maisha ya watu binafsi, Jumuiya na Jamii katika ujumla wake. Baba Mtakatifu Francisko anakazia pia dhana ya majadiliano katika ukweli na uwazi. Amani ni kiini cha mafundisho makuu ya dini mbali mbali duniani.

Kwa Wakristo, amani ni zawadi ambayo Mwenyezi Mungu aliwakirimia wanadamu kama inavyojionesha wakati wa Fumbo la Umwilisho pamoja na Ufufuko wa Kristo. Zawadi ya kwanza ambayo Mitume walibahatika kupata kutoka kwa Yesu Mfufuka ni amani, ambayo iliwaletea mageuzi katika maisha yao, wakawa tayari kutoka kifua mbele kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka wafu. Hii ni zawadi ambayo inawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni vyombo na wajenzi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.