2015-06-03 16:32:00

Leo hapa ni pilika pilika majichano kwenda mbele! Ikirudi ni pancha!


Katika mji mmoja kulikuwa na tajiri mwenye jumba zuri la ghorofa. Katika ghorofa hiyo kulikuwa na chumba kikubwa alichokuwa anakikodisha bure kwa ajili ya tafrija mbalimbali ikiwepo minuso ya arusi au hafla mbalimbali za kidini. Lakini tajiri huyo alikuwa mtu wa kawaida kabisa, mpole, mnyeyekevu na mwenye upendo. Daima alikuwa tayari kusaidia wengine. Kitu cha kushangaza zaidi hakuwa anaona kigagasi kufanya shughuli za kitumishi au za akinamama, ikiwa ni pamoja na kufagia nyumba, kuokota kuni za kupikia, kwenda mtoni kuchota maji nk. Machoni pa wengi hasa kwa wabantu tajiri huyu angeweza kufikiriwa labda amelishwa ”limbwata”. Kumbe hapana, yeye alifanya hivi kutokana tu na utu, upendo na unyenyekevu aliokuwa nao. Ndugu zangu, tajiri kama huyu ndiye anayefumba mada ya fikara tutakayoitafakari katika somo la leo.

Fasuli ya Injili yetu ya leo imegawanyika sehemu mbili. Sehemu ya kwanza ni maandalizi ya pahala pa tafrija ya Pasaka ya Wayahudi, yaani hapa ni patashika nguo kuchanika!  Sehemu ya pili ni tafrija yenyewe na yote yaliyojiri. Kabla ya kuziangalia sehemu hizo kinaganaga hatuna budi kuangalia mambo mengine mawili. Mosi, mazingira ya Yesu na kikundi chake yalivyokuwa kwa mfano ukiangalia kwa makini sehemu ya kwanza ya fasuli ya leo (Mk. 14:12-16) unahisi mara moja kwamba Yesu na kikundi chake walikuwa wanapigwa vita sana na viongozi wa serikali na dini. Hata hivyo katika kipindi hiki iliwabidi wawe Betania (Yerusalemu) ili kula Kondoo wa Pasaka. Aidha kuhusu maandalizi ya Pasaka, yaonekana Yesu alishayapanga pahala pakufanya karamu na alijua anachotaka kukifanya. Kadhalika alitambua pia kuwa mjini kunakaa watu matajiri na wanajulikana kwa ubinafsi wao. Lakini alijua pia kuwa kuna matajiri wengine wazuri, wenye utu na maadili mema.

Jambo la pili, hatuna budi kuviangalia vipengee vingine vitatu vinavyoelezwa katika sehemu hii ya kwanza: Mosi, tunadokezewa kuwa chokochoko za kusherekea Pasaka hazikuanzishwa na Yesu, bali na Mitume ndiyo maana wanamwuliza Yesu: “Ni wapi utakapo tuende tukuandalie uile Pasaka?” (Mk. 14:12). Hoja ya mitume kufanya uchokozi huu ni kwa sababu wao ndiyo waliotaka kula Pasaka ya Wayahudi, kwa vile walizoea kufanya kila mwaka ili kukumbua uhuru wao toka Misri na kukumbuka Agano walilolifanya na Mungu juu ya mlima Sinai.

Kipengele cha pili yule mwanaume aliyebeba mtungi na kukutana na wanafunzi wawili kama alivyoagiza Yesu. “Nendeni zenu mjini atakutana nanyi mwanamume amechukua mtungi wa maji, mfuateni popote atakapokingia nanyi mtamwuliza” (Mk 14:13) Yaonekana mwanaume huyu ni tajiri hadi amekuwa na jengo la ghorofa lenye chumba kikubwa. Aidha yaonekana Yesu amemtaja hapa kwa lengo maalumu. Ama kweli mwanaume huyu anapewa kipao mbele kwa kitendo chake cha kubeba mtungi wa maji akiwatangulia mitume kuingia jumba la ghorofa na kuwaonesha chumba cha karamu. Fumbo lililojificha hapa ni hili kwamba Yesu anataka kubadilisha fikra za wanafunzi wake wote tukiwepo wewe na mimi juu ya mtazamo wa mambo katika jamii. Yaani kubadilika jinsi ya kuuona utajiri, kwamba hata tajiri anaweza kuwa mtakatifu na kutuongoza wengine kumwendea Yesu.

Katika kesi hii anawaongoza mitume kuingia kwenye jengo kutakakoadhimishwa Ekaristi Takatifu. Kadhalika tunafundishwa jinsi ya kuwatendea kwa haki wanawake, watumishi na watu wanyonge katika jamii. Mungu anatutaka tutumikiane. Aidha anataka kuanzisha utamaduni mpya kwamba katika chumba cha Karamu ya Yesu (Ekaristi) anaingia mtu yule anayeweza kuona watu kwa namna tofauti, kama vile tajiri mnyenyekevu, mwenye utu, kujifanya mdogo, yaani wanaume kuamua kutumikia na kufanya kazi za kitumishi, au kazi wanazodhani ni za kike.

Kipengee cha tatu ni jinsi kilivyoelezwa kile chumba cha sherehe: “Naye mwenyewe atawaonyesha orofa kubwa imeandikwa tayari, humo tuandalieni.” (Mk 14:15). Hivi hata aina hii ya chumba ilikuwa mawazoni mwa Kristu. Yasemwa kwamba chumba kilikuwa ghorofani. Hapa upate picha ya kilele cha mlima ambako sauti ya Bwana au Neno lake likisemwa lisikike hadi mbali kama Mungu alivyofanya kwa Musa juu ya mlima Sinai (Kut. 24:1-4). Aidha ukubwa wa chumba unamaanisha kujaza watu wa kila aina bila kumbakiza mtu yeyote nje. Mandhali hii ya karamu inatupatia pia picha ya Misa Takatifu (Ekaristi). Sehemu hii ya kwanza ya injili inatusindikiza na kutuingiza hadi chumbani mwa karamu ambako mitume na Yesu wameketi wanakula sikukuu ya Pasaka. Humo karamuni mitume walikuwa na wazo moja tu nalo ni la kusherekea Uhuru wao toka utumwani Misri na kusherekea Agano la Sinai.

Katika sehemu ya pili ya Injili (Mk 14: 22-26) tunaona upepo ndani ya chumba unabadilika ghafla: “Nao walipokuwa wakila Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa.” Maneno hayo yaliyotanguliwa kabla na sala yalikuwa yamezoeleka kusikika. Lakini baada ya maneno hayo kitendo kilichofuata ndicho kilichowaacha solemba mitume hasa pale wanapoona wanalengwa wao na wanaambiwa: “Chukueni na mle.” Kama vile haikutosha, wanashtuka zaidi wanapoona mkate wa kawaida unavyopata thamani ya pekee pale Yesu anaposema: “Huu ni mwili wangu,” yaani “Mkate unageuzwa kuwa nafsi yenye mwili.” Yaani mwalimu wao anajizawadi maisha yake yote kwa wanafunzi wake kama mkate. Yaani, anawataka nao wawe nafsi moja naye na kushiriki maisha yake. Kumbe mradi wa Mungu ulikuwa ni kuileta mbingu hapa duniani. Kumleta Mungu kwa binadamu yaani, kutusamehe dhambi kwa kujitoa mwenyewe kama bwana arusi anavyojitoa kwa bi arusi wake.

Yesu anahitimisha Karamu kwa kuchukua kikombe kilichojaa divai (kama vile wanavyogongeana glass za bia wanaarusi) anasema: “Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili wengi”. Tendo hili nalo limejaa alama nyingi kwa sababu ya maneno yafuatayo. “Amin nawaambia ninyi, sitakunywa tena kabisa uzao wa mzabibu, hata siku ile nitakapounywa mpya katika ufalme wa Mungu.” (Mk. 14:25). Yaonekana leo Yesu ameishiana kabisa na Agano la kale. Hapa unapata picha kuwa Yesu yuko arusini kama alivyokijibu kikundi cha mafarisayo na cha wanafunzi wa Yohane Mbatizaji waliomwuliza, kwa nini wanafunzi wake hawafungi: “Walioalikwa arusini wawezaje kufunga maadamu bwana arusi yupo pamoja nao? Muda wote walipo na bwana arusi pamoja nao hawawezi kufunga. Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi, ndipo watakapofunga siku ile.” (Mk. 2:19-20).

Ujumbe huu unaeleweka, kwamba pahala asipokuwa Yesu (bwana arusi), hapo hapana divai na hivi hapajachangamka. Lakini Yesu atakapowagawia watu wote divai yake hapo ndipo anapopasemea kwamba: “Nitakunywa nanyi  divai mpya katika ufalme wa Mungu.”  Kwa hiyo, Agano lilotolewa mlima Sinai lililenga kuwaunganisha Waisraeli (Taifa) na Bwana Mungu, kwani lilitiwa muhuri kwa damu ya wanyama, iliyokuwa na nguvu fulani. Lakini Agano la Yesu linatiwa muhuri kwa damu ya kimungu na inatolewa kwa kila mtu. Aidha damu ya Agano Jipya “imemwagika kwa ajili ya wote.” Kwa sababu Ekaristi haikuwekwa kwa ajili ya kumkutanisha mtu binafsi na Kristu au kutuliza matakwa binafsi au ubinafsishaji wa kiroho, la hasha bali, ni chakula cha jumuia, ni mkate uliomegwa na kugawana kwa jumuia iliyozaliwa baada ya ufufuko wa Kristo.

Mlango wa jumba la sherehe uko wazi kwa wote. Karamu ya ufalme wa Mungu iliyotabiriwa na manabii, imeandaliwa “kwa ajili ya mataifa yote” (Isaya 25:6). Wote wanakaribishwa, matajiri na maskini, wagonjwa na wazima. Kwa upande wa Mungu hakuna binadamu aliye safi na mchafu, anayestahili na asiyestahili. Mbele ya Ekaristi sisi sote tu wadhambi, hatustahili, lakini tumealikwa kuingia na kujumuika na Kristo.  Mkate ambao ni Kristu, na kalisi ya damu yake inatufanya tuwe damu moja naye na kati yetu pia, na tunaunga ukoo mmoja wa taifa moja walio na sheria moja ya kusaidiana na kutumikiana kindugu katika upendo, utu na heshima.

“Chochote mlichomtendea mmoja wa hawa ndugu zaidi walio wadogo, mmenitendea mimi” (Mt. 25:40). Ubinadamu ni mwili wa Mungu. Kwa hiyo hatuwezi kamwe kutenganisha mwili wa Kristu ulio Altareni ndani ya Kanisa na mwili wa Kristo ulio katika Altare ya ndugu, katika maskini, kwa wanaoteseka, kwa wagonjwa, kwa wakimbizi, kwa wazee, kwa wapweke, na kwa yeyote aliye katika matatizo. Ekaristi ni nguvu katika safari ya unyonge na unyenyekevu, inanifanya niwajibike na kuwa mwangalifu kwa mwili na damu ya ndugu aliye barabarani na katika maisha yangu ya kila siku. Kwa sababu Bwana arusi amejifanya bwana arusi kwa ndugu mdogo. Tufuate na kuiga unyenyekevu wa mwanaume anayebeba mtungi na kuingia jumba la karamu ya Kristo.

Heri kwa Sikukuu ya Ekaristi Takatifu.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.