2015-06-03 08:01:00

Kweli watu wamekengeuka, badala ya kujenga amani wanajigamba kwa mauaji!


Patriaki Bartolomeo wa kwanza anaridhishwa na hatua za makusudi zilizochukuliwa na Serikali ya Ufaransa kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ili kujadili kw akina na mapana hatima ya Wakristo huko Mashariki, kundi ambalo linaendelea kuuwawa kikatili, kunyanyaswa na kudhulumiwa. Kwa kipindi kirefu, Jumuiya ya Kimataifa ilionekana kulifumbia macho tatizo hili. Ni matumaini ya viongozi wa Kanisa kwamba, Umoja wa Mataifa utaweza kusitisha haraka iwezekanavyo mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, ili haki, amani na maridhiano yaweze kutawala tena katika maisha ya watu.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza ameyasema haya hivi karibuni katika ujumbe aliowaandikia washiriki wa kongamano la kimataifa lililokuwa linafanyika mjini Bari, Kusini mwa Italia kuhusu hatma ya Wakristo huko Mashariki ya Kati, lililokuwa limeandaliwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yenye makao yake makuu mjini Roma. Kutoweka kwa Wakristo huko Mashariki ya Kati ni janga la kibinadamu na uharibifu mkubwa wa historia na ustaarabu wa watu, kwani uwepo wa Wakristo huko Mashariki ya kati si bahati mbaya bali ni sehemu ya mpango wa Mungu kwa mwanadamu.

Mauaji, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo, ni tatizo la kimataifa kwani kuna Wakristo sehemu mbali mbali za dunia wanaoendelea kuuwawa na kunyanyasika kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, jambo ambalo si haki kabisa. Hapa kuna mabadiliko makubwa katika maisha ya kiroho, watu badala ya kujenga upendo na mshikamano wa dhati, wanajikita katika mauaji ya watu wasiokuwa na hatia. Hizi ni dalili za kukengeuka kwa mwanadamu, kimaadili na kiutu.

Wakristo Mashariki ya kati ni warithi amini wa Ukristo, tamaduni na mapokeo mbali mbali, kumbe hawa ‘hawa si watu wa kuja” kama wanavyodhani wengine na kwamba, hawana haki ya kuishi huko Mashariki ya Kati. Ni watu ambao wanahifadhi kumbu kumbu ya dhati mioyoni mwao na kwamba, kwa miaka mingi wameishi kwa amani na maridhiano na waamini wa dini ya Kiislam na kwamba, misimamo mikali ya kiimani ni jambo hatari na kamwe haliwezi kukubalika na wapenda amani kwani linatishia usalama, amani na mfungamano wa kijami kati ya watu.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anabainisha kwamba, uwepo endelevu wa Wakristo huko Mashariki ya Kati unategemea kwa namna ya pekee dhamana na mchango wao wa kuwa ni daraja la upatanisho kati ya watu wa dini mbali mbali, tayari kujikita katika misingi ya haki, amani na maridhiano, kwa kuzingatia na kuheshimu uhuru wa kuabudu.

Mauaji ya kinyama wanayofanyiwa Wakristo huko Mashariki ya Kati ni changamoto kwa Wakristo kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika damu ya mashhuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake. Madhulumu na nyanyaso za kidini ni mambo ambayo yanafumbatwa katika majadiliano ya kiekumene kwa Wakristo wa nyakati hzi. Kinzani na magumu wanayokabiliana nayo Wakristo kinaweza kuwa ni kipindi muafaka cha kufanya mageuzi ya kiekumene, kwani katika damu na machozi, Wakristo wote kwa pamoja wanatambua hatima ya maisha yao, kiasi cha kugundua pia machozi ya masikitiko kutokana na kugawanyika kwa misingi ya kihistoria, badala ya kuwa wamoja chini ya Kristo mchungaji mwema.

Askofu mkuu Brian Farrel, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa linalohamasisha Umoja wa Wakristo amefafanua kwa kina mapana kuhusu changamoto za kiekumene zinazoendelea kujitokeza miongoni mwa Wakristo huko Mashariki ya kati. Tofauti za: Makanisa na Madhehebu ya Kikristo zinakubalika miongoni mwa Wakristo kama sehemu ya utambulisho wao wa kitamaduni, kikabila na kijiografia zinazopata mwangwi wake, tangu mwanzo kabisa wa Ukristo huko Mashariki ya Kati. Kutokana na mwelekeo huu, Wakristo huko Mashariki ya Kati wanajisikia kuwa kweli ni ndugu wamoja katika Kristo, wanaounda Familia ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.