2015-06-03 08:19:00

Fumbo la Ekaristi Takatifu ni chemchemi ya upendo, umoja na mshikamano


Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Upendo, zawadi ya Yesu Kristo kwa Kanisa lake na sadaka ambamo yeye mwenyewe anajisadaka kwa ajili ya uhai na maendeleo ya Kanisa lake. Ni Sakramenti ya Altare, ambamo  Yesu anakutana na wafuasi wake na hivyo kuanza safari ya pamoja, tayari kuwashibisha wafuasi wake na kuzima kiu ya maisha yao ya kiroho.

Ekaristi Takatifu ni Fumbo la imani linalopaswa kusadikiwa kwani hii ndiyo kazi ya Mungu kwa kumwamini Yesu aliyetumwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Huu ni Mkate ulioshuka kutoka mbinguni, zawadi ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Yesu Kristo ni mwanakondoo wa kweli na sadaka ya Baba wa mbinguni anayefunga Agano Jipya na la Milele. Ekaristi Takatifu ni kanuni msingi ya uwepo na maendeleo ya Kanisa. Ekaristi inajenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa Kanisa; ni kiungo thabiti na Sakramenti zote za Kanisa.

Hivi ndivyo Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa kumi na sita anavyoandika katika Waraka wake wa Kitume kuhusu Ekaristi Takatifu kama Sakramenti ya Upendo “ Sacramentum Caritatis”. Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania katika maadhimisho ya Siku kuu ya Ekaristi Takatifu kwa mwaka huu 2015 linawaalika waamini kuondokana na utandawazi usioguswa na mahangaiko ya watu kutokana na vita, nyanyaso na dhuluma ambazo wakati mwingine zinatendwa kwa misingi ya udini.

Watu hawana budi kutubu na kumwongokea Mungu na kwamba, maadhimisho sahihi ya Fumbo la Ekaristi Takatifu yanayojikita katika Ibada na uchaji ni nyenzo muhimu sana katika kupambana na utandawazi usioguswa na mahangaiko ya jirani, tayari kujenga na kudumisha mshikamano wa upendo na udugu, unaomwalika mwamini kuwa kweli ni sadaka kwa ajili ya jirani zake, hasa wale maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Maaskofu wanasema kwamba, hii ni changamoto endelevu ili kuweza kukabiliana na utamaduni wa kifo usiojali wala kuguswa na kilio cha watu wasiokuwa na hatia. Waamini watumie maadhimisho ya Siku kuu ya Ekaristi Takatifu kujenga mahusiano ya dhati na Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka kwa wafu, tayari kujisadaka kwa ajili ya ustawi na mafao ya jirani zao sehemu mbali mbali za dunia. Lengo ni kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu, dhidi ya ubinafsi na uchoyo unaoendelea kuota mizizi katika mioyo ya watu.

Maaskofu Katoliki Hispania wanawaalika Waamini kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema katika kukuza na kudumisha majadiliano, haki na amani, upendo na mshikamano katika mapambano dhidi ya baa la njaa na umaskini; ilikuhakikisha kwamba, chakula kinapatikana kwa kila binadamu. Kwa maneno mengine, Maaskofu wanawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kushiriki kikamilifu katika kuchangia kwa hali na mali kampeni ya Caritas inayopania kuwawezesha watu wengi kuwa na uhakika wa usalama wa chakula katika maisha yao. Hii ni changamoto ya kuendelea kushikamana na watu wasiokuwa na fursa za ajira, wanaoteseka na kunyanyasika kiasi cha kushindwa kutekeleza dhamana na majukumu katika familia zao. Waamini wasimame kidete kupambana na utumwa mamboleo pamoja na biashara haramu ya viungo vya binadamu; mambo yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Kwa namna ya pekee, Mama Kanisa anapojiandaa kusherehekea Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, waamini wanahamasishwa kuwa kweli ni vyombo na wajumbe wa huruma ya Mungu kwa kuwamegea jirani zao upendo na huruma inayobubujika kutoka kwa Mungu mwenyewe, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.