2015-06-02 09:43:00

Watoto wanaoishi na wazazi gerezani wakutana na Baba Mtakatifu Francisko


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 30 Mei 2015 amekutana na kuzungumza na watoto 200 kutoka sehemu mbali mbalali za Italia, waliofika mjini Vatican kwa treni maalum, hii ikiwa ni awamu ya tatu, tukio ambalo liliandaliwa na Baraza la Kipapa la utamaduni kama sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kitamaduni na watu mbali mbali. Hawa ni watoto ambao wanaoishi na wazazi wao wanaotumikia adhabu gerezani. Kauli mbiu ya mkutano huu wa aina yake na Baba Mtakatifu ni “kuruka”, ili kuwapatia watoto hawa faraja katika shida na mahangaiko yao ya kila siku.

Watoto wengi walioshiriki katika mkutano huu wanakiri kwamba, pengine hii ni mara yao ya kwanza na ya mwisho kuweza kuonana na kuzungumza na Baba Mtakatifu uso kwa uso, kiasi cha kusahau shida na mahangaiko yao ya kila siku katika maeneo ya magereza. Watoto wamewashukuru pia wazazi wao ambao wamewapatia ruhusa ya kushiriki katika mkutano huu pamoja na Baba Mtakatifu Francisko aliyewapatia matumaini mapya kwa kuthamini utu na heshima yao kama binadamu.

Wengi wa watoto hawa kwa mara ya kwanza wamepanda Treni kutoka sehemu mbali mbali za Italia ili kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu, tukio ambalo kwa wengi wao limebakiza chapa ya kudumu katika akili na mioyo yao. Huduma ya kichungaji kwa wafunga magerezani ni utume ambao unapaswa kupewa msukumo wa pekee, ili kuwaonjesha wafungwa matumaini ya maisha mapya. Mara nyingi ni watu wanaojisikia kutengwa na kudhalauliwa na jamii, kumbe, nafasi ya kuonana uso kwa uso na Baba Mtakatifu si haba, ni tukio muhimu sana katika maisha yao.

Wafungwa wanapaswa kupokelewa na kupewa nafasi nyingine tena katika maisha yao, ili kutubu, kuongoka na kuanza hija ya maisha yanayojikita katika matumaini, wakiwa tayari pia kusamehe. Kwa watoto wanaoishi na wazazi wao ambao wanatumikia adhabu gerezani, imekuwa ni siku kuu ya aina yake, kila mtoto amebaki na kumbu kumbu ya kudumu moyoni na akilini mwake.

Baba Mtakatifu amewataka watoto hawa kushikamana na Yesu Kristo wanaporuka katika safari ya maisha yao, ili kweli waweze kuwa huru, vinginevyo wanaweza kujikuta kwamba, wanakuwa na mioyo migumu kama jiwe na kugandamana ndani mwao kama barafu. Baba Mtakatifu amewaonesha moyo wa upendo na huruma ya kibaba, akiwauliza maswali na wao wakijitahidi kuyajibu kwa furaha na bashasha kubwa.

Baba Mtakatifu amewataka watoto hawa kuendelea kuwa na ndoto ya maisha mapya licha ya magumu wanayokabiliana nayo kutokana na wazazi wao kutumikia vifungo gerezani. Watoto waendelee kusali na kusikiliza Neno la Mungu, ili kuweza kukutana na Yesu anayewafariji katika shida na mahangaiko yao ya ndani. Neno la Mungu linawawezesha kukua na kukomaa. Watoto hawa wamempatia Baba Mtakatifu shairi ambalo linamwelezea Yesu kuwa rafiki wa wenye dhambi; kwa mateso, kifo na ufufuko wake, awajawezeshe kupata amani na kuwaokoa kutoka katika dhambi, ili waweze kuzaa matunda ya upendo, haki na ukweli. Hivi ndivyo watoto hawa walivyopenda kumshirikisha Baba Mtakatifu ndoto ya maisha yao, huku wakiwa wanaruka pamoja na Yesu anayewahakikishia usalama wa maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.