2015-06-02 10:57:00

Wanawake jifungeni kibwebwe kuwainjilisha Watu wa Mataifa!


Yesu Kristo mara baada ya kukamilisha utume wake hapa duniani, aliwakabidhi mitume dhamana na ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa kuwabatiza watu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu ili waweze kupata wokovu na maisha ya uzima wa milele. Yesu anatambua udhaifu na mapungufu ya wafuasi wake, anafahamu fika ukosefu wa rasilimali katika utekelezaji wa dhamana hii, lakini bado anawatia moyo na ari ya kusonga mbele kwa imani na matumaini.

Yesu aliamua kuwachagua wafuasi wake, akawapatia dhamana hii nyeti pamoja na kuwahakikishia kwamba, Roho Mtakatifu atawakumbusha na kuwafundisha ukweli wote juu ya Fumbo la Msalaba, watakapokuwa wanakutana na watu wa nyakazi mbali mbali, huku wakiwatangazia Habari Njema ya Wokovu. Ikumbukwe kwamba, Roho Mtakatifu ndiye mhusika mkuu katika dhamana ya Uinjilishaji. Ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee anawaalika waamini kuwaonjesha ndugu zao huruma na upendo wa Mungu, mambo msingi yaliyofunuliwa na Yesu katika maisha na utume wake.

Waamini wanapaswa kuwa wanyenyekevu na watiifu kwa Roho Mtakatifu, wakitambua na kuthamini Fumbo la Utatu Mtakatifu, linalowawezesha kuwa kweli na imani thabiti, wajasiri, watu huru na wenye kutekeleza dhamana na utume wao kwa njia ya ugunduzi. Ni mahubiri yaliyotolewa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwa washiriki wa Semina ya wanawake ndani ya Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake, waliokuwa wanashiriki semina ya kimataifa iliyoandaliwa na Gazeti la L’Osservatore Romano linalomilikiwa na Vatican.

Imekuwa ni fursa kwa wanawake kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuchambua kwa kina na mapana fursa, matatizo na changamoto ambazo zinawakabili wanawake na wasichana sehemu mbali mbali za dunia wanapotekeleza dhamana na wajibu wao ndani na nje ya Kanisa. Ibada hii ya Misa imeadhimishwa, hapo tarehe 31 Mei 2015 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Catherina wa Siena, lililoko mjini Roma. Huyu ni mtakatifu aliyebahatika kulitafakari kwa kina Fumbo la Utatu Mtakatifu, akalitolea ushuhuda makini unaomwilishwa katika upendo, akashiriki kwa dhati Fumbo la Kristo lililomwezesha kuwa kweli ni mtu huru.

Mtakatifu Catherina wa Siena alikuwa jasiri na mwenye kulipenda Kanisa, kiasi hata cha kutoa changamoto ya kufanya mabadiliko ya kina katika maisha na utume wa Kanisa. Akaonesha kwamba, Mungu ni chemchemi ya upendo na huruma kwa viumbe wake. Kwa njia ya haki ameweza kuwaosha dhambi zao kwa Damu azizi ya Yesu Kristo. Upendo wa Mungu kwa waja wake hauna mipaka, ni upendo ambao unapaswa kumwilishwa kwa jirani, kwani binadamu hawezi kupenda kama anavyopenda Mungu. Upendo kwa Mungu na jirani ni kipimo ambacho kitatumika wakati wa hukumu ya siku ile ya mwisho!

Ni matumaini ya Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwamba, wanawake katika hija na maisha yao hapa duniani, kwa njia ya mwanga wa Injili, wanaweza kupambana bila kukata tamaa na matatizo pamoja na changamoto wanazokabiliana nazo katika maisha yao; wakiwa huru kama watoto wateule wa Mungu, wanaweza kuonja ushindi wa Kristo, unaofumbatwa katika huruma, tayari kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya Furaha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.