2015-06-02 10:27:00

Wakurugenzi wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa waanza mkutano Vatican


Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu pamoja na Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mwambata na Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa wamefungua rasmi mkutano mkuu wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa, Jumatatu, tarehe Mosi, Juni 2015 unaofanyika katika awamu kuu mbili. Sehemu ya kwanza inagusia masuala ya kichungaji na sehemu ya pili inajikita katika maisha na utume wa Kanisa. Jinsi ya kulitegemeza Kanisa leo na kesho ndiyo mada inayoongoza mkutano huu.

Kwa namna ya pekee, Kardinali Filoni katika hotuba yake elekezi amekazia umuhimu wa kutembea pamoja na Kanisa katika matukio mbali mbali ya maisha na utume wake; mambo msingi ya kuzingatiwa; ushirikiano na mshikamano wa kimissionari; ushirikiano na udugu wa Kikanisa, changamoto za kiuchumi na jinsi ya kuhamasisha maadhimisho ya Siku ya Kimissionari Duniani inayoadhimishwa Jumapili ya mwisho ya mwezi Oktoba, kila mwaka.

Kardinali Filoni anabainisha kwamba, maadhimisho ya mkutano mkuu wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa unaohudhuriwa na wakurugenzi wa Mashirika haya kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ni kielelezo cha udugu na umoja katika mchakato wa kuunda Familia moja ya Watu wa Mungu. Huu ni mwaliko wa kuendelea kusimama kidete kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, licha ya vita, nyanyaso na madhulumu yanayoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia.

Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa yanatekeleza dhamana yake, ili kuendeleza utume wa Kanisa wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Itakumbukwa kwamba, Kanisa ni alama na chombo cha wokovu, mwaliko hata kwa Makanisa mahalia kushirikishana na kugawana rasilimali watu, vitu na fedha kama kielelezo cha mshikamano wa Kikanisa.

Kardinali Filoni anasema kwamba, Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kiwe ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani ili kukumbatia huruma na upendo wa Mungu. Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, iwe ni fursa kuhamasisha tena mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko; unaojikita katika kweli za Kiinjili, Upendo na Unabii; mambo msingi kwa ajili ya watu wa kizazi hiki.

Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni mwaliko kwa waamini kutoka katika ubinafsi wao kwa kuwafungulia na kuwaonjesha wengine Injili ya Furaha; Faraja na matumaini kwa wafungwa na wale ambao wanatumbukizwa katika utumwa mamboleo; ili kuwarudishia tena utu na heshima yao kama binadamu. Hii ni fursa kwa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa ari na moyo mkuu.

Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Waraka kuhusu kazi za kimissionari za Kanisa, “Ad Gentes”, tema itakayopembuliwa kwa kina na mapana wakati wa maadhimisho ya mkutano mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu kwa mwaka 2015. Ni mwaliko wa kufanya tafakari ya kina ili kubainisha fursa, matatizo na changamoto zilizopo katika mchakato wa Uinjilishaji mpya pamoja na kukazia mwelekeo wa kimissionari. Mkutano huu pia ni fursa ya kushirikishana uzoefu, mang’amuzi na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa Kanisa.

Kardinali Filoni anaendelea kukazia umuhimu wa ushirikiano wa kimissionari kama sehemu ya mchakato makini wa Uinjilishaji, kwa kuliwezesha Kanisa kuwa kati ya watu kwa ajili ya watu na maendeleo yao kiroho na kimwili. Watu waendelee kufundwa vyema ili wajisikie kweli ni sehemu ya Kanisa, tayari kuchangia kwa hali na mali. Katika miaka ya hivi karibuni, mchango wa waamini kutoka katika Makanisa ya Ulaya umepungua kwa kiasi kikubwa.

Kumbe, kuna haja kwa Makanisa mahalia kushirikiana ili kutekeleza mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita kwa namna ya pekee katika kuhamasisha: ari na moyo wa kimissionari; kwa kuwafunda wamissionari na kuendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na taasisi zinazohudumia Makanisa mahalia, ili kuwa na ugawaji bora zaidi wa rasilimali fedha na watu. Umefika wakati kwa Makanisa mahalia kuonesha mshikamano wa kidugu kwa kusaidiana kwa hali na mali kadiri ya uwezo uliopo. Utunzaji na matumizi ya mali ya Kanisa hauna budi kufanywa kwa kuzingatia: ukweli, uwazi, uaminifu na weledi. Fedha ya Kanisa itumike katika miradi iliyokusudiwa na wala si vinginevyo.

Maadhimisho ya Siku ya Kimissionari Duniani, iwe ni kilele cha kuhamasisha ari na mwamko wa shughuli za kimissionari zinazofanywa na Mama Kanisa katika kipindi cha Mwezi Oktoba kila mwaka. Wakurugenzi wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa wanapaswa kuhamasisha maadhimisho haya katika ngazi mbali mbali, ili waamini wengi waweze kushiriki na kuchangia kwa hali na mali.

Kardinali Fernando Filoni anakumbusha kwamba, Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa yana dhamana na wajibu wa kutoa ruzuku kwa Balozi za Vatican sehemu mbali mbali za dunia, kwani hii ni huduma inayopania kujenga mahusiano na Makanisa mahalia. Balozi hizi ndizo zinazohakiki matumizi ya fedha zinazotumwa kwenye Makanisa mahalia.  Wakurugenzi wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa ni wadau muhimu katika mchakato wa Uinjilishaji unaotekelezwa kwenye Makanisa mahalia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.