2015-06-02 15:26:00

Ninakuja kwenu kama mjumbe wa amani, majadiliano na upatanisho!


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa Familia ya Mungu nchini Bosnia na Erzegovina anasema, hapo tarehe 6 Juni 2015 anatarajiwa kuwashirikisha furaha yake kwa kutembelea mji wa Sarayevo. Anakwenda kati yao kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani sanjari na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga na kuimarisha amani na maridhiano nchini humo.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuungana pamoja naye katika sala, ili hija hii ya kitume iweze kuzaa matunda yanayokusudiwa na Jumuiya ya Kikristo na Jamii katika ujumla wake. Hija hii ya kitume inaongozwa na kauli mbiu “Amani iwe kwenu”. Haya ni maneno ambayo Yesu Kristo mfufuka aliwaambia Mitume wake waliokuwa wanejifungia kwenye Chumba cha juu, Jioni ile ya Pasaka. Yesu ni nguvu na matumaini kwa waja wake, anawajalia amani, ili kuweza kumpokea katika mioyo na kuwashirikisha wengine amani hii kwa njia ya furaha na upendo.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, kwa sasa anajiandaa kwenda kuwatembelea kama ndugu na mjumbe wa amani, ili kuwaonjesha wote heshima na urafiki wake. Anataka kuwatangazia watu wote huruma, wema na upendo wa Mungu kwa binadamu. Anapenda pia kuwahakikishia wananchi wote wa Bosnia na Erzegovina uwepo wake wa karibu kwa njia ya kiroho.

Anawahimiza Wakatoliki kuwa kweli ni mashuhuda wa imani na upendo unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya amani, maridhiano na ushirikiano wa dhati. Baba Mtakatifu anasema, anasubiri kwa hamu kukutana na wananchi wote wa Bosnia na Erzegovina na kwa sasa anapenda kuwapatia baraka yake ya kitume pamoja na kuwaweka chini ya ulinzi na tunza na Bikira Maria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.