2015-06-01 09:35:00

Mchakato wa mapambano dhidi ya baa la umaskini Barani Afrika!


Wafanyabiashara, wachumi na wanafunzi kwa muda wa siku mbili wameshiriki kikamilifu katika kongamano la kimataifa la uchumi wa mshikamano lililoandaliwa na Chama cha kitume cha Wafokolari kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kikatoliki Afrika Mashariki na Kati, CUEA. Mradi wa uchumi wa mshikamano ni dhana iliyoanzishwa na Mama Chiara Lubich kunako mwaka 1991, alipokuwa nchini Brazil kama sehemu ya mchakato wa mapambano dhidi ya baa la umaskini linaloendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Ni  mwaliko wa kuhamasisha wadau mbali mbali katika sekta ya uchumi kuhakikisha kwamba, wanatumia rasilimali watu, mali na fedha kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya jirani zao kwa kutengeneza fursa za kazi na ajira hususan mingoni mwa vijana. Akihojiwa na Radio Vatican kutoka Nairobi, Liliane Mugombozi, mkurugenzi wa Jarida la New City Afrika anakiri kwamba, hii imekuwa ni fursa kwa wafanyabiashara, wachumi na wanafunzi kukutana na kubadilishana uzoefu na mang’amuzi yao kutoka sehemu mbali mbali za dunia, katika mchakato wa kupambana na baa la umaskini.

Dhana ya uchumi wa mshikamano inafanyiwa kazi sehemu mbali mbali za dunia kadiri ya mazingira na vipaumbele vya watu. Wamepata nafasi ya kusikiliza uzoefu unaojikita katika mtindo wa maisha na tamaduni za watu; mambo msingi yanayomwilishwa katika mchakato wa kazi na utekelezaji wa mikakati mbali mbali ya shughuli za kiuchumi. Jambo ambalo limetiliwa mkazi ni ushirikiano wa umoja, upendo na udugu kati ya wafanyakazi ili kuongeza tija na ufanisi kazini.

Utu na heshima ya binadamu vinapewa msukumo wa pekee katika mikakati na sera za uzalishaji mali na utoaji wa huduma; sanjari na utunzaji bora wa mazingira; mambo ambayo kimsingi yanaweza kusaidia kuokoa gharama katika shughuli za uzalishaji na matokeo yake, fedha hii inasaidia katika mchakato wa maboresho ya uzalishaji na utoaji wa huduma.

Lengo si kupata faida kubwa, bali ni kuhakikisha kwamba, huduma za kiuchumi zinakuwa endelevu zaidi kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye shida na mahangaiko mbali mbali, ili kugawana utajiri na rasilimali mbali mbali ambazo Mwenyezi Mungu amewawekea mbele yao. Hiki ndicho kielelezo cha uchumi wa mshikamano unaopania pamoja na mambo mengine, mafao ya wengi.

Liliane Mugombozi anasema kwamba,  katika athari za myumbo wa uchumi kimataifa, wafanyabiashara na wachumi hawana haja ya kukata tamaa. Huu ni wakati ambao wanapaswa kunoa akili zao zaidi ili kutafuta rasilimali itakayowawezesha si tu kupata faida, bali kuwajengea watu imani na matumaini ya maisha bora zaidi. Mifano mbali mbali ya uchumi wa mshikamano imeoneshwa, kiasi kwamba, imekuwa ni kielelezo makini cha kupambana na ujinga kwa kuwapeleka watoto shulen pamoja na kuboresha huduma kwa wagonjwa.

Huu ni wajibu ambao umetekelezwa na wafanyabiashara na wachumi waliokuwa na uwezo, wakaona umuhimu wa kushirikiana na jirani zao katika kupambana na umaskini, njaa na ujinga, ili kuwajengea watu nguvu ya kiuchumi, itakayowawezesha kununua bidhaa na huduma zinazozalishwa na kutolewa na wafanyabiashara hawa. Mkutano huu umefanyika Jijini Nairobi, ili kuwawezesha wafanyabiashara, wachumi na wasomi kuanza kujenga dhana ya uchumi wa mshikamano kama sehemu ya mchakato wa maboresho ya maisha ya jirani zao. Itakumbukwa kwamba, tamaduni nyingi Barani Afrika zinajipambanua kwa moyo wa ushirikiano na mshikamano, kwa ajili ya mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.