2015-06-01 08:55:00

Iweni na ujasiri wa kukataa sera na mifumo inayohatarisha maisha ya ndoa!


Furaha ya familia ndiyo kauli mbiu iliyokuwa ikifanyiwa kazi kwa ushrikiano kati ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM pamoja na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, CCEE kuanzia tarehe 29 hadi 31 Mei, 2015, huko Maputo, Msumbiji. Semina hii imewashikisha wajumbe 35 kati yao, Maaskofu ni 22. Askofu mkuu Francisco Chimoio, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji aliwakaribisha wajumbe wa semina hii na baadaye wakapata historia fupi ya maisha na utume wa Kanisa Katoliki nchini Msumbiji.

Askofu mkuu Edgar Parra Pena, Balozi wa Vatican nchini Msumbiji, amepongeza ushirikiano ambao umeoneshwa na Mashirikisho haya mawili ya Maaskofu wa Afrika na Ulaya katika kukabiliana na changamoto za kijamii, kichungaji na kitaalimungu katika Mabara yao. Anasema, kuna matatizo na kinzani kubwa ambazo familia sehemu mbali mbali za dunia zinakabiliana nazo. Huu ni mwaliko kwa Kanisa kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, linajikita katika mchakato wa Uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha.

Waamini wawe mstari wa mbele katika kushuhudia na kutangaza tunu msingi za Injili ya Familia. Kanuni maadili na utu wema ni kati ya mambo ambayo yanapaswa kukaziwa katika maisha ya ndoa na familia, ili kukabiliana na wimbi kubwa la kumong’onyoka kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zinazoendelea kuenea kwa kasi hata wakati mwingine kwa njia ya sheria za nchi.

Askofu mkuu Gabriel Mbilingi, Rais wa SECAM, kwa ufupi, amebainisha changamoto zilizojitokeza wakati wa maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya familia iliyofanyika mjini Vatican kunako mwaka 2014. Anazihamasisha familia kuwa kweli ni kielelezo cha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia pamoja na kuwa na ujasiri wa kukataa sera na mikakati inayohatarisha maisha ya ndoa kadiri ya mpango wa Mungu.

Kanisa kwa upande wake, halina budi kutoka kimasomaso ili kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia inayojikita katika utamaduni wa upendo kamili kati ya bwana na bibi, ili kuenzi na kuendeleza Injili ya uhai na wala si vinginevyo. Dhamana hii inapaswa kutekelezwa kwa umakini mkubwa kwa kuzingatia mchakato wa utamadunisho, makini na wenye ufanisi unaosafisha na kuboresha mila, tamaduni na mapokeo ya watu mintarafu tunu msingi za Kiinjili.

Ujumbe wa Yesu Kristo ni chombo makini kinachoweza kukabiliana kikamilifu na changamoto za maisha ya ndoa na familia zinazoendelea kumsumbua mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Askofu mkuu Gabriel Mbilingi amelitaka Kanisa kufanya maamuzi magumu ya mikakati ya shughuli za kichungaji ili kuokoa na kuendeleza familia ambayo kwa sasa inaandamwa na majanga makubwa katika maisha na utume wake.

Kardinali Peter Erdo, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, katika ujumbe uliosomwa kwa niaba yake na Askofu Duarte da Cunha, Katibu mkuu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, amegusia changamoto zinazojitokeza katika maisha na utume wa familia kutokana na ukanimungu na ubinafsi unaoingizwa katika familia kwa kasi ya ajabu. Anasikitika kusema kwamba, idadi ya waamini wanaofunga ndoa ya Kikristo inazidi kupungua mwaka hadi mwaka.

Hii ni changamoto kubwa kwa mihimili ya Uinjilishaji kuhakikisha kwamba, inawasaidia wanandoa kuishi vyema wito wao kadiri ya mpango wa Mungu pamoja na kuendelea kuwahamasisha vijana wa kizazi kipya kufanya maamuzi machungu katika maisha yao kwa kukataa kishawishi cha uchumba sugu, dhana ambayo inazidi kukua na kukomaa kwani watu hawataki kuwajibika katika maamuzi wanayoyafanya katika maisha yao.

Kardinali Erdo anasema, licha ya changamoto na magumu yanayojitokeza katika maisha na utume wa ndoa na familia, lakini inafurahisha kuona kwamba kuna vyama vya kitume vinavyoanzishwa na familia ili kuonesha mshikamano wa kiimani, kwa kusindikizwa na Kanisa pamoja na familia nyingine za Kikristo. Anasema, Kanisa Barani Ulaya linaheshimu na kuvutiwa sana na ushuhuda wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zinazojionesha Barani Afrika. Anaiomba Familia ya Mungu Barani Afrika kuendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na Kanisa Barani Ulaya, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu na ustawi wa wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.