2015-05-30 17:50:00

Wakurugenzi wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa waanza mkutano Roma


Mkutano mkuu wa Mwaka wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa unaanza rasmi Jumatatu tarehe 1 Juni 2015 kwa kuhudhuriwa na Marais pamoja na Makatibu wakuu wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa. Sehemu ya kwanza ya mkutano huu itajadili kuhusu mikakati na shughuli za kichungaji na sehemu ya pili itazungumzia masuala ya kawaida ya Mashirika haya ya Kipapa.

Mkutano huu unatarajiwa kufunguliwa na Kardinali Fernando Filoni Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu pamoja na Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mwambata na Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa. Mkutano huu unaongozwa na kauli mbiu “Jinsi ya kutegemeza utume wa Kanisa leo na kesho” Mada itakayochambuliwa na Kardinali Orlando Quevedo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cotobato, Ufilippini.

Makatibu wakuu wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa watatoa taarifa ya mwaka pamoja na makadirio ya bajeti. Wataangalia maombi ya ruzuku kutoka kwenye Makanisa mahalia yaliyowasilishwa kwenye Mashirika haya.  Tarehe 5 Juni 2015 wajumbe wanatarjiwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Wakurugenzi wakuu wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa kutoka katika Makanisa mahalia watatoa taarifa pamoja na kupembua utekelezaji wa maamuzi yaliyofikiwa kwenye mkutano uliopita. Askofu mkuu Protase Rugambwa, anatarajiwa kufunga mkutano, Jumamosi, tarehe 6 Juni 2015.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.